Waziri mkuu wa Libya aliyetekwa nyara sasa yuko huru
10 Oktoba 2013Serikali ya Libya imesema kuwa tukio la kutekwa nyara huenda lilikuwa ni ulipizaji kisasi dhidi ya kitendo cha kikosi cha jeshi la Marekani mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mwanaharakati mmoja anayehusika na kundi la al-Qaeda alikamatwa katika mitaa ya mji huo mkuu.
Kutekwa nyara kwa Ali Zeidan kunaakisi udhaifu mkubwa katika serikali ya Libya , ambayo inashikiliwa mateka na wanamgambo , wengi wao wanatoka katika makundi ya wapiganaji wa Kiislamu.
Wanamgambo hao wanasemekana kuwa wamekasirishwa na hatua ya jeshi la Marekani kumkamata mtuhumiwa, anayehusika na kundi la al-Qaeda, ambaye anafahamika kama Abu Anas al-Libi, na wanaishutumu serikali kwa kuruhusu kikosi hicho cha Marekani ama kushirikiana nacho kumkamata mtuhumiwa huyo.
Wavamia hoteli
Watu walioshuhudia wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa zaidi ya watu 150 waliokuwa na silaha wakiwa katika magari ya pikup waliizingira hoteli ya Corinthia kabla ya majira ya alfajiri leo.
Kundi kubwa la watu hao liliingia katika jengo hilo la hoteli, baadhi wakisalia katika eneo la kupokelea wageni wakati wengine walielekea katika ghorofa ya 21 ambako Zeidan alikuwa akiishi.
Watu hao wenye silaha waliwafunga pingu walinzi wa waziri huyo mkuu kabla ya kumkamata na kuondoka nae, amesema mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwasababu ya kuhofia usalama wake.
Wamesema kuwa Zeidan hakutoa upinzani wowote wakati akiongozwa kuelekea katika magari ya watu hao.
Mtafaruku wa uongozi
Katika ishara ya mtafaruku nchini Libya , kukamatwa kwa Zeidan kumeelezwa na duru mbali mbali kuwa ama ni kuwekwa kizuwizini, ama ni utekaji nyara, unaoakisi jinsi wanamgambo wanavyoingiliana na mfumo wa uongozi ambao hauko pamoja nchini Libya.
Mohamed Shaaban , meneja wa usalama katika hoteli hiyo ya Corinthia, amesema kuwa watu hao wenye silaha wameuonyesha uongozi wa hoteli hiyo waranti wa kukamatwa kwa waziri mkuu huyo , ambao wamedai umetolewa na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali.
Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali imesema haijatoa waranti kwa kukamatwa Zeidan.
Wakati polisi na jeshi la nchi hiyo hayako katika hali nzuri, wanamgambo huorodheshwa kutumika kama walinzi wa usalama katika mashirika ya serikali , licha ya kuwa utiifu wao uko kwa makamanda wao badala ya maafisa wa serikali na mara kadha wameweza kuwatisha maafisa. Wanamgambo wanatokana na vikosi ambavyo vimepigana katika vuguvugu la kuuangusha utawala wa kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, na mara kadha wanatambulika kama "wanamapinduzi".
Lakini hivi punde mbunge katika bunge la Libya amesema kuwa waziri mkuu huyo ameachwa huru na wanamgambo waliomteka leo alfajiri.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri: Yusuf Saumu