1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe atarajiwa kuwasili Teheran

Oumilkheir Hamidou
12 Juni 2019

Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe anatarajiwa kuwasili mjini Teheran kwa ziara ya aina pekee ya masaa 24 akijipa matumaini ya kupunguza mvutano kati ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran na Marekani.

https://p.dw.com/p/3KDYt
Japan Staatsbesuch l US-Präsident Donald Trump trifft Japanischen Ministerpräsidenten Shinzo Abe
Picha: picture alliance/dpa/MAXPPP

Waziri mkuu Shinzo Abe  ambae ndege yake inatarajiwa kutuwa jioni, ni kiongozi wa kwanza wa serikali ya Japan kuitembelea Iran tangu mapinduzi ya mwaka 1979 yaliyomng'owa madarakani Shah.

Japan ni mshirika muhimu wa Marekani, na wakati huo huo ina uhusiano mzuri na wa jadi pamoja na Iran.

"Katika wakati ambapo jumuia ya kimataifa imeingiwa na wasi wasi kutokana na mivutano inayozidi makali Mashariki ya kati, Japan inataraji kufanya iwezalo kwaajili ya amani na utulivu katika eneo hilo" amesema Shinzo Abe mbele ya waandishi habari kabla ya kuondoka mjini Tokyo.

Waziri mkuu wa Japan amepangiwa kukutana na rais Hassan Rouhani wa Iran na baadae pamoja na kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamanei. Anasema  anataraji kuwa na "mazungumzo ya dhati" pamoja na viongozi hao wawili.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Zarif alipokutana na waziri mkuu Shinzo Abe mjini Tokyo mwezi May uliopita
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Zarif alipokutana na waziri mkuu Shinzo Abe mjini Tokyo mwezi May uliopitaPicha: picture-alliance/dpa/Kyodo/MAXPPP

Iran kuiomba Japan ipatanishe

Iran pia inasema itaiomba Japan ipatanishe  ili Marekani ipunguze makali ya vikwazo dhidi yake. "Afisa mmoja wa serikali ya Iran ameliambia shirika la habari la Reuters. Na afisa mwengine amemtaja waziri mkuu Abe kuwa "mpatanishi bora zaidi anaeweza kurahisisha hali ya mambo."

Akiwa katika ziara ya siku nne nchini Japan, mwezi uliopita, rais wa Marekani Donald Trump alikaribisha msaada wa Shinzo Abe katika suala la Iran.  Hata hivyo maafisa kadhaa wa Japan wanasema waziri mkuu Shinzo Abe anakwenda Tehran bila ya orodha ya madai wala ujumbe kutoka Washington.

Mvutano kati ya Washington na Teheran umezidi makali mnamo wiki za hivi karibuni, mwaka mmoja baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya mwaka 2015 ya kimataifa kuhusu mradi wa nuklea wa Iran. Na kuanzia mwezi uliopita wa Mei serikali ya mjini Washington imezidisha makali ya vikwazo dhidi ya Iran  na kuzitaka nchi zote na makampuni yote yaache kuagizia mafuta ya Iran la sivyo yatafutwa katika mfumo wa fedha wa kimataifa.

Marekani imetuma pia idadi zaidi ya wanajeshi na manuari za kivita kukabiliana na kile wanachokitaja kuwa "kitisho kutoka Iran.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga