Waziri mkuu wa Japan atangaza kujiuzulu.
2 Juni 2010Matangazo
Akizungumza na wabunge wa chama chake cha Democratic Party of
Japan -DPJ-, katika kikao maalum kwenye bunge la nchi hiyo, Waziri
Mkuu wa Japan Yukio Hatoyama alisema kwamba atajiuzulu, huku
akitaka kuundwa upya kwa chama hicho.
Amemtaka pia Katibu mkuu wa chama chake Ichiro Ozawa kujiuzulu
na kusema kwamba Katibu Mkuu huyo amekubali ombo hilo.
Kushuka kuungwa mkono kwa baraza lake la mawaziri kumekuja
baada ya kuvunja ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za
uchaguzi, ya kuhamisha kituo cha jeshi la majini la Marekani kutoka
katika kisiwa cha Okinawa.
Waziri mkuu huyo pia anakabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka
ajiuzulu kutoka katika chama chake cha Democratic Party of Japan -DPJ.
Hatoyama ambaye amekuwa waziri mkuu wa nne wa Japan katika
kipindi cha miaka minne aliuambia mkutano mkuu wa chama hicho
kwamba anastaafu kwa sababu ya kujiondoa kwa chama cha Social
Democratic SDP, katika serikali ya muungano.
Chama hicho kilijiondoa siku ya Jumapili baada ya Hatoyama
kuamua kuendelea kukiacha kituo cha jeshi la Marekani katika
kisiwa kilichoko kusini mwa Japan.
Uamuzi huo ulikuja baada ya Waziri mkuu Yukio Hatoyama
kumfukuza siku ya Ijumaa kiongozi wa chama hicho cha Social
Democratic Party -SDP- Mizuho Fukushima katika nafasi yake ya
Waziri anayeshughulikia masuala ya jinsia, baada ya Bibi Fukushima
kukataa kuidhinisha makubaliano juu ya kuhamishia makao mapya
kituo hicho cha kijeshi cha Marekani.
Chama tawala nchini Japan cha Democratic Party of Japan -DPJ-
kinatarajia kufanya mkutano mkuu siku ya Ijumaa kuweza kuamua juu
ya kiongozi mwingine ajaye.
Chama hicho cha DPJ kina wabunge wengi katika bunge, ambalo
ndio linachagua waziri mkuu.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wabunge wengi wa chama hicho
cha Kidemokrasia cha DPJ, walipinga uchaguzi wa mwezi ujao wa
bunge wakimtaka Waziri Mkuu huo kujiuzulu.
Aidha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa walionya kuwa chama
hicho tawala kitashindwa katika uchaguzi kama hali haitabadilika.
Upepo wa kisiasa uligeuka ghafla tofauti na wakati serikali hiyo mpya
iliposhika madaraka ikiwa na umaarufu mwezi Septemba, baada ya
chama cha DPJ kushinda kwa kishindo chaguzi mkuu wa mwezi
Agusti mwaka jana.
Kabla ya uchaguzi huo mkuu uliofanyika mwaka uliopita, Hatoyama
aliahidi kuendeleza uhusiano ulio sawa na Marekani, nchi ambayo ni
mshirika mkuu wa Japan, hujku akiwasisitizia wakazi wa kisiwa cha
Okinawa kwamba hataruhusu kituo kingine cha kijeshio cha Marekani
kujengwa katika kisiwa chao, lakini wiki iliyopita, serikali yake ilikubali
ombi la Marekani kuhamishwa tena kituo katika eneo lisilo na watu
wengi katika kisiwa hicho cha Okinawa licha ya upinzani uliokuwepo.
Mwandishi: Halima Nyanza(dpa)
Mhariri:Mtullya Abdu
Matangazo