Waziri Mkuu wa Japan asema Olimpiki sio kipaumbele
10 Mei 2021Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga amesema leo kuwa hajawahi kuiweka mbele michezo ya Olimpiki, huku uchunguzi wa maoni ukionyesha kuwa karibu asilimia 60 ya watu nchini Japan wanataka tamasha hilo lifutwe ikiwa ni chini ya wiki 11 kabla ya kufunguliwa rasmi.
Maafisa wa kimataifa wa Olimpiki, waandalizi wa michezo hiyo ya Tokyo, na Suga mwenyewe wamesisitiza kuwa mashindano hayo yataendelea katika njia salama. Watazamaji hawataruhusiwa na waandalizi wametoa msururu wa kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Suga amewaambia wabunge kuwa kipau mbele chake ni kuyalinda Maisha na afya ya watu wa Japana. Lazima wazuie maambukizi ya corona.
Amesema Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC ina kauli ya mwisho kuhusu Michezo hiyo na jukumu la serikali ni kuchukua hatua ili iandaliwe kwa njia salama.
Waandalizi wa Tokyo 2020 wamesema jana kuwa ziara ya mkuu wa IOC iliyotarajiwa Mei 17 hadi 18 imefutwa, kutokana na kurefushwa kwa hali ya dharura wiki iliyopita na masuala mengine yanayoikabili Japan.
AFP; Reuters