Waziri mkuu wa Japan kufanya majadiliano ya wazi na Trump
29 Novemba 2024Waziri mkuu wa Japan Shigeru Ishiba, amesema atakuwa na majadiliano ya wazi na rais mteule wa Marekani Donald Trump, na kuongeza kuwa ushirikiano kati yao ni muhimu katika kuhakikisha kuwepo kwa eneo huru na wazi la pasifiki.
Wakati akitoa hotuba muhimu ya sera katika bunge la nchi yake, Ishiba amesema;
"Kwa kawaida, Marekani ina maslahi yake ya kitaifa sawa na Japan na ndio maana nafikiri kubadilishana maoni kwa uwazi na kuimarisha maslahi ya kitaifa ya nchi zote mbili kwa njia ya ushirikiano kutasaidia kufikia kuwepo kwa eneo hilo huru na wazi la pasifiki."
Soma: Biden akutana na washirika wake wa Japan na Korea Kusini
Ishiba, anayejieleza kujitolea katika ulinzi, ametoa wito wa kuundwa kwa jumuiya ya kujihami ya NATO barani Asia itakayoongozwa na kanuni kwamba shambulio la mmoja ni shambulio kwa wote.
Wakati huo huo, waziri huyo mkuu amesema Marekani inapata manufaa makubwa ya kimkakati kutokana na kuwepo kwa vifaa na maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vyake nchini Japan.