1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya juu yasema uteuzi wake umekiuka katiba

10 Septemba 2015

Waziri mkuu wa Guinea Bissau Baciro Dja ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo baada ya mahakama ya juu nchini humo kutengua uteuzi wake kwa maelezo ya kuwa uteuzi huo umekiuka katiba.

https://p.dw.com/p/1GU9i
Waziri mkuu wa Guinea Bissau aliyejiuzulu Baciro Dja
Waziri mkuu wa Guinea Bissau aliyejiuzulu Baciro DjaPicha: picture-alliance/dpa/L. Fonseca

Uamuzi huo uliofanywa na jopo la majaji wanane unaofuatiwa na hatua hiyo ya kujiuzulu unatishia kuvuruga jitihada za taifa hilo la Afrika ya magharibi za kuondokana na mapinduzi ya kijeshi na misukosuko ya kisiasa.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo yenye kurasa 15 uteuzi huo wa Dja uliofanyika mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu haukukidhi viwango kadhaa vya kikatiba.

Rais wa nchi hiyo Jose Mario Vas alimteua bwana Dja kushika nafasi hiyo ya Uwaziri mkuu ikiwa ni wiki moja tu baada ya kumfuta kazi Domingos Simoes Pereira kufuatia mfululizo wa migongano kadhaa ya kiutendaji , ikiwa ni pamoja na uteuzi wa mkuu mpya wa majeshi wa nchi hiyo.

Chama tawala pia chapinga uteuzi huo

Uamuzi huo hivi sasa unamuweka Rais wa nchi hiyo katika mzozo na chama chake tawala ambacho kilipinga hatua hiyo na kusema kuwa ni sawa na kuipindua katiba kwani uteuzi huo ulipaswa kupata mashauriano toka kwa vyama vinavyounda bunge la nchi hiyo.

Guinea-Bissau Parlament
Bunge la Guinea BissauPicha: DW/T. Camará

Uamuzi wa Vaz wa kumfuta kazi waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Domingos Simoes Pereira, ulikataliwa na wajumbe wengi wa chama tawala cha PAIGC ambacho wote hao wawili ni wanachama.

Rais Vaz alimteua Dja kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo na kufuatiwa na uteuzi wa baraza la mawaziri juma hili ambapo sasa hukumu hiyo ya mahakama ya juu inaibua maswali juu ya uhalali wa baraza hilo la mawaziri.

Waziri mkuu huyo aliyejiuzulu amesikika pia akivishutumu vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo kwa kutangaza mijadala ya moja kwa moja toka ndani ya bunge la nchi hiyo katika kipindi cha migogoro na kusema kuwa havikuheshimu mwongozo uliotolewa kuhusiana na kulinda kuwepo kwa hali ya amani.

Dja alikuwa ni waziri wa ulinzi katika serikali ya Rais Carlos Gomes Junior aliyepinduliwa mnamo mwaka 2012.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/RTRE

Mhariri : Yusuf Saumu