Waziri Mkuu wa Ethiopia aizuru Eritrea
8 Julai 2018
Kwenye uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, Waziri Mkuu Abiy amepokelewa na Rais Afwerki, huku wakikumbatiana na kuangua kicheko. Kuwasili kwake kumeonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya taifa ya Eritrea. Kundi kubwa la watu lilikuwa kando likiimba na kucheza huku wakivalia fulana zenye picha za viongozi hao wawili.
Ziara hii inafanyika mwezi mmoja baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuwashangaza wengi, alipoamua kuyatambua kikamilifu makubaliano yaliyomaliza vita vya mpaka baina ya nchi hizo ndugu, ambavyo vilidumu kwa miaka miwili. Ethiopia na Eritrea zimekuwa hazana uhusiano wa kidiplomasia tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka 1998. Abiy mwenyewe alipigana katika mojawapo ya miji ambayo imekuwa kiini cha mzozo kati ya nchi hizo.
Juhudi za amani ya kudumu
Fitsum Arega ambaye ni kiongozi wa ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia, amesema kupitia mtandao wake wa twitter kwamba ziara ya Waziri Mkuu Abiy ina ''malengo ya kuimarisha juhudi za kufikia amani ya kudumu'' katika ya nchi hizo za Upemba wa Afrika.
''Mataifa yetu mawili yana historia moja, na yanafungamana kwa namna ambayo siyo rahisi kuipata mahali pengine'' amesema Fitsum, na kuongeza kuwa huu unaweza kuwa mwanzo wa kumaliza miongo miwili ya kukoseana imani, na kuchukua mtazamo mpya.
Balozi wa Eritrea nchini Japan Estifanos Afworki, amesema, yeye pia kupitia mtandao wa twitter, kwamba hakuna kiongozi yeyote mwingine aliyepokelewa kwa furaha mjini Asmara kama Abiy Ahmed.
Upendo usio kifani
Waethiopia walioandamana na waziri wao mkuu katika ziara hii nchini Ethiopia, wameelezea kushtushwa na mapenzi waliyoonyeshwa. Mmoja wao amesema ilikuwa kama ndoto.
Kutambua makubaliano ya kumaliza vita na Eritrea ulikuwa uamuzi mkubwa zaidi miongoni mwa hatua nyingi za mageuzi alizozichukuwa Waziri Mkuu Abiy tangu kuingia madarakani Aprili mwaka huu. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42 tayari amewaachia waandishi wa habari na wapinzani kutoka gerezani, na ameufungua uchumi wa nchi hiyo ambao kwa sehemu kubwa umekuwa ukidhibitiwa na serikali.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape.rtre
Mhariri: John Juma