Waziri mkuu wa China asema ghasia za Tibet zinachochewa na watu wa nje
18 Machi 2008Waziri Mkuu wa China anadai kuwa ghasia za jimbo la Tibet zilipangwa na kuchochewa na mataifa pamoja na makundi ya kigeni yanayomuunga mkono kiongozi wa kidini wa Kibudhaa,ambae anaishi uhamishoni Dalai Lama.
Matamshi haya pamoja na matokeo ya sasa ya Tibet yanatoa wasiwasi kuhusu kufanyika kwa mazumnguzo kati ya utawala wa Beijing na kiongozi huyo wa kidini.
Mjumbe mmoja wa upande wa kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama kwenye mazungumzo kati yao na serikali ya China,ambayo yamekuwa yakiendelea kwa mda sasa,amesema kuwa,hatua ya Beijing ya kutumia nguvu kupita kiasi wakati ikikabaliana na waandamanaji katika mjini mkuu wa jimbo hilo wa Lhasa inatia wasiwasi.Watibeti walioko uhamishoni, wanaopinga serikali ya China, wanadai kuwa takriban watu 80 ndio waliuawa katika kamatakamata hiyo-madai yanayopingwa na serikali ya China inasema ni watu 13 tu.
Mjumbe huyo,Bhuchung Tsering, masema kuwa, kamata kamata ya juzi imeleta wasiwasi ya kutojulikana mwelekeo wa mazungumzo yao.
Mara ya mwisho pande hizo kukutana ulikuwa wakati wa kiangazi na walikutana China kwa duru ya sita ya mazunguzo.Wakati huo wajumbe wa Dalai Lama waliweka wazi kuwa wanachotaka ni utawala wa ndani.
Lakini leo waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, amesema kuwa China itafanya mazunguzo na Dalai Lama ikiwa itaachana na madai yake ya kuitaka Tibet kujitenga.
Lakini yeye Dalai Lama mwenyewe anasema hawataki kujitenga bali wao wanachotaka ni utawala fulani wa ndani.
Lakini waziri mkuu wa China amesema kuwa wao wamesha weka mambo yao wazi kuwa wako tayari kufanya mazungumzo ya maana nae almradi tu atambue kuwa Tibet ni sehemu ya China ilioungana.
Yeye Bhuchung, amesema kuwa suala hilo litabaki kuwa mchongoma kwa serikali ya China hadi pale matatizo ya Watibet yote yatakapopatiwa ufumbuzi.
Amebaini kuwa maandamano ya sasa yamesambaa kwingineko kuliko yale ya mwaka wa 1987.
Marekani imekuwa inaoongoza miito ya kuitaka serikali ya China kukaa kwa meza moja na Dalai Lama ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa Tibet.
Waziri mkuu wa China amesema kuwa ghasia za Tibet zinachochewa na makundi yanaounga mkono Dalai Lama.
Kwa mda huohuo,Tibet kwenyewe siku ya jumanne kumeripotiwa kuwa kutulivu baada ya mda uliotolewa na serikali ya China huko Tibet ya kuwataka waandamanaji kujisalimisha,la sivyo watakipata cha mtema kuni.
Dalai Lama alitoroka eneo lake la Tibet mwaka wa 1959 baada ya utawala wa Beijing kuyavunja maasi.
China inachukulia utawala wake wa Tibet ulioanza mwaka wa 1950 kama hatua ya kulikomboa eneo hilo na kuwaepusha watu wa Tibet ukandamizaji wa kitemi.