Serikali imewalipa walalamikaji fidia ya dola 50milioni
27 Novemba 2017Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau juzi amewaomba radhi watu wa kabila la Newfoundland na wa jimbo la Labrador kutokana na unyanyasaji uliofanyika katika shule za bweni katika karne yote ya 20.
``Tupo hapa leo kuomba radhi kutokana na makosa ya kihistoria´´ alisema akiomba radhi kwa unyanyasaji wa kingono, kimwili na kisaikolojia uliofanyika katika shule tano za jimbo hilo.
``Huu ndiyo ukweli mgumu katika historia ya Canada.`` alisema
Kitendo cha TRUDEAU kuomba radhi kumekuja katika wakati ambapo serikali hiyo imeruhusu kuchukuliwa kwa hatua za kisheria baada ya malalamiko kuletwa na wanafunzi wa zamani 900 wa shule hizo. Wengi wakiwa ni wale walioondolewa kwa nguvu katika jamii zao na kutengwa na familia zao katika jitihada ya kulazimishwa kubadilika na kuingia katika tamaduni zenye wafuasi wengi.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times la Marekani, walalamikaji hao walilipwa jumla ya dola milioni 50 za Canada kama fidia.
Katika sherehe hizo, zilizofanyikia HAPPY VALLEY-GOOSE Bay, pamoja na Trudeau alikuwepo pia Tony Obed, mwanafunzi wa zamani wa shule hizo za bweni , aliyeongoza harakati za kufunguliwa mashtaka hayo.
Obed,ambaye alisimulia hadharani kuhusu unyanyasaji wa kingono aliofanyiwa akiwa shule alikubali hatua ya kuombwa na serikali ya Canada.
Mauaji ya kitamaduni
Ni kama mauaji ya utamaduni, kwani mabadiliko hayo ya utamaduni yalifanyika kwa kiasi kikubwa Marekani na Canada katika karne ya 19 na ya 20. Huko Canada baadhi yao walivumilia hadi mwaka 1996.
Nchini Canada, shule nyingi zilikuwa zikisimamiwa na serikali na wakati mwingine zilisimamiwa na wamishionari au wahisani.
Wakati Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Stephen Harper alipoomba radhi kwa mitandao ya shule hizo mnamo mwaka 2008, hakuzitaja shule za Newfoundland na Labrador kutokana na kwamba hazikuwa sehemu ya Canada hadi mwaka 1949.
Tume ya upatanisho na ukweli iliyoundwa baada ya Harper kuomba radhi, ilibaini kuwa uvunjwaji wa haki uliofanywa katika shule hizo za bweni ni sawa na mauaji ya kimbari ya tamaduni.
Utafiti uliofanywa mwaka 2016 na Wanazuoni wa Kituo cha Mbadala wa Sera cha nchini Canada, ulibaini kuwa asilimia 60 ya watoto wenye asili ya aborigine katika maeneo ya ndani nchini humo wanaishi katika umaskini na kitakwimu, idadi kubwa ya wanawake ndiyo waliokuwa waathirika wakubwa wa mauaji nchini Canada.
Mwandishi: Florence Majani
(Mhhttp://www.dw.com/en/trudeau-sorry-for-historic-wrong-against-aboriginal-canadians/a-41527614)
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.