Waziri mkuu Shinzo Abe adhamiria kubadili katiba
22 Aprili 2007Japan inakusudia kubadili katiba yake ili kuiwezesha nchi hiyo kushiriki kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kijeshi ya kimataifa. Hayo amesema waziri Mkuu wa nchi hiyo bwana Shinzo Abe kabla ya kuanza ziara anayotarajia kufanya Marekani wiki hii.
Waziri Mkuu Abe ameeleza hayo katika mahojiano na magazeti ya Washington Post na Newsweek kabla ya kuanza ziara ya Marekanai ambapo atafanya mazungumzo na rais Bush.Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala kadhaa ya kimataifa yanayozihusu nchi zao ikiwa pamoja na makusudi ya Japan juu ya kubadili katiba yake inayoepusha dhima za kijeshi. Katiba hiyo inaiwekea Japan vizingiti kadhaa katika sekta ya kijeshi.
Katika mahojiano hayo waziri mkuu wa Japan amesemaa kuwa ni wajibu wa kila mwanasiasa wa nchi yake kufikiria juu ya nini Japan inaweza kufanya ili kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuleta utengamavu na amani siyo tu kwa ajili ya Japan bali pia kwa dunia nzima.
Tokea kumalizika vita kuu vya pili Japan imekuwa inajiweka kando inapohusu kutimiza dhima za kimataifa katika sekta ya kijeshi.
Lakini sera hiyo imeanza kubadilika mnamo miaka ya karibuni.
Nchi hiyo ilipeleka wanajeshi 600 nchini Irak ili kushiriki katika shughuli za kuijenga nchi hiyo upya. Wanajeshi hao waliwekwa kusini mwa Irak ambapo kwa jumla pana utulivu wa kiasi. Hatahivyo wanajeshi hao tayari wamesharudishwa nyumbani.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tokea kumalizika vita kuu vya pili kwa majeshi ya Japan kupelekwa katika nchi inayokabiliwa na mzozo wa kivita.
Ikiwa ni nchi inayoshika nafasi ya pili katika kuufadhili Umoja wa Mataifa Japan imeshashiriki katika majukumu kadhaa ya kulinda amani kwa niaba ya Umoja huo.Majeshi ya nchi hiyo yameshiriki katika majukumu ya kulinda amani nchini Cambodia na kwenye milima ya Golan ambapo ina askari wapatao alfu 5 na mia saba.
Japan pia ilipeleka majeshi nchini Thailand na Indonesia ili kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na athari zilizosababishwa na kimbunga cha Tsunami mnamo mwaka 2004.
Hadi mwaka huu nchi hiyo ilikuwa na idara ya ulinzi tu lakini sasa idara hiyo imebadilishwa na kuwa wizara kamili ya ulinzi.Hatua hiyo inaashiria dhamira ya serikali ya waziri mkuu Abe ya kujinasua na katiba inayoiwekea nchi hiyo vizingiti.
Japan inataka kuondokana na katiba iliyowekwa kwa agizo la Marekani baada ya kumalizikka vita kuu vya pili.Juu ya hayo waziri mkuu wa Japan bwana Abe amesema kuwa katiba ya sasa ina vipengele vilivyopitwa na wakati.
Mazingira ya usalama ya Japan na ya dunia nzima yamebadilika sana ameeleza bwana Abe, amesema kuwa silaha za maangamizi zimeongezeka duniani.
Sambamba na hayo pana harakati za kupambana na ugaidi na kwamba migogoro inazuka hapa na pale.
Kabla ya kuanza ziara yake nchini Marekani wiki hii ambapo atajadili masuala hayo na rais George Bush, waziri mkuu wa Japan amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inatarajia nchi yake itoe mchango zaidi katika kuzikabili changamoto za kimataifa, amesema katiba mpya ya nchi yake lazima iende sambamba na mahitaji ya karne hii ya 21.
Licha ya kuwapo wasiwasi miongoni mwa nchi fulani barani Asia, Marekani siku zote imakuwa inaihimiza Japan juu ya kushiriki kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kijeshi nje ya mipaka yake.