1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waziri Mkuu mpya wa Japan Fumio Kishida aidhinishwa na bunge

Sylvia Mwehozi
4 Oktoba 2021

Waziri mkuu mpya wa Japan Fumio Kishida ameitisha uchaguzi wa bunge Oktoba 31 na kuapa kuimarisha njia za kukabiliana na janga la virusi vya corona, muda mchache baada ya kuidhinishwa na wabunge kuchukua wadhifa huo.

https://p.dw.com/p/41FOV
Japan | Fumio Kishida zum neuen Premierminister gewählt
Picha: Eugene Hoshiko/AP/dpa/picture alliance

Baraza la chini la bunge limemwidhinisha Kishida mwenye umri wa miaka 64 kuchukua mikoba ya Yoshihide Suga kama waziri mkuu na kuungwa mkono kwa wingi na kura za muungano wa vyama tawala. Kishida ambaye aliwahi kuwa waziri wa zamani wa mambo ya nje kwa miaka mingi chini ya utawala wa waziri mkuu Shinzo Abe, ameteua baraza la mawazi lenye sura ngeni kwa kuwaondoa wote kasoro waziri wa mambo ya nje Toshimitsu Motegi na yule wa ulinzi Nobuo Kishi.

Uamuzi wake wa kuitisha uchaguzi umekuja kwa mshangao, ingawa awali ulipangwa kufanyika Novemba 28 wakati muhula wa bunge la sasa ukimalizika Oktoba 21. Bunge la sasa litavunjwa Oktoba 14. Kishida amesema kuwa atazingatia malipo ya misaada ya COVID-19, akiongeza kuwa amewaelekeza mawaziri wanaoshughulikia janga hilo kuja na sera kuhusu chanjo na kuimarishwa kwa mfumo wa kimatibabu na kuongeza upimaji ili kusaidia kufungua uchumi.

Japan | Fumio Kishida - Wahl zum Parteivorsitzenden der LDP
Waziri Mkuu mpya Fumio Kishida na Yoshihide Suga aliyemaliza muda wakePicha: Carl Court/REUTERS

"Watu wengi wana wasiwasi kwamba hata kama hali imeimarika, idadi ya maambukizi inaweza kupanda na kama hospitali zitaweza kumudu", aliwaeleza waandishi wa habari.

Wakosoaji wanaona baraza lake ambalo limejumuisha wanawake watatu kama ishara ya mwendelezo badala ya mwanzo mpya.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae In amempongeza Kishida katika barua iliyoelezea matumaini kwamba mataifa hayo mawili yatakuwa mfano katika ushirikiano kama nchi jirani. Seoul imesema kwamba iko tayari kushirikiana na baraza jipya la Japan katika masuala ya uchumi, utamaduni na mabadilishano baina ya mtu na mtu.

Rais Joe Biden pia amempongeza Kishida akielezea muungano wa Marekani -Japan kama "msingi" katika amani na utulivu wa kikanda. Rais wa China Xi Jinping naye ametuma salamu za pongezi na kusema kuwa ana matumaini ya uhusiano wa kirafiki na ushirika na Japan.