Waziri Mkuu Maliki aongoza katika uchaguzi wa Iraq
8 Machi 2010Wakati huo huo chama cha waziri mkuu wa zamani, Iyad Allawi, kinachotenganisha dini na siasa, kinashika nafasi ya tatu. Chama hicho kinaungwa mkono na Wairaqi wengi wa madhehebu ya Kisunni ambao ni wachache na wamepoteza ushawishi katika serikali ya al-Maliki inayodhibitiwa na Washia walio wengi.
Na katika eneo la Wakurdi, kaskazini mwa Iraq, chama kipya kilichoundwa na mpenda mageuzi, Goran, kinashindana na chama cha PUK cha Rais Jalal Talabani. Kundi hilo jipya huenda likapunguza nguvu za PUK na KDP vilivyodhibiti katika uwanja wa kisiasa wa Wakurdi tangu miongo kadhaa. Katika siku zilizopita, mshikamano wa vyama hivyo ulisaidia kuwapa sauti Wakurdi katika siasa za Iraq.
Hivi sasa nchini Iraq, kwa sehemu kubwa, makundi yaliyokuwa yakiwakilisha jamii kwa ukabila na dini yamesambaratika. Baadhi ya makundi hayo yamevuka mipaka ya kidini na upo uwezekano wa makundi hayo kuanzisha majadiliano ya kuunda serikali mpya ya muungano, ikiwa hata chama kimoja hakitojinyakulia wingi katika bunge lenye viti 325. Majadiliano kama hayo ni mtihani kwa demokrasia dhaifu nchini Iraq, huku Marekani ikitazamia kupunguza kwa nusu idadi ya wanajeshi wake na kusitisha operesheni za kijeshi ifikapo tarehe 31 mwezi Agosti.Rais wa Marekani, Barack Obama, ameazimia kuwarejesha nyumbani wanajeshi wote wa Marekani kutoka Iraq ifikapo mwisho wa mwaka 2011.
Maafisa wa Marekani wanasema mpango huo unaweza kuhatarishwa, ikiwa tu hali ya usalama itadhoofika nchini Iraq. Kwa maoni ya mtaalamu David Mack wa Taasisi ya Mashariki ya Kati, katika nchi kama Iraq haitoshi kushinda uchaguzi tu, kinachohitajiwa ni uongozi wenye ufanisi.
Mwandishi: Prema Martin/Reuters/AFP
Mhariri: Miraji Othman