Waziri mkuu Brown atangaza Mei 6 uchaguzi Uingereza
6 Aprili 2010Waziri-mkuu Gordon Brown wa Uingereza ametangaza leo huko 10 Downing Street, mjini London , kuwa Waingereza watakwenda kupiga kura mwezi ujao- Mei 6. Hivyo, waziri-mkuu Brown, ameanzisha kampeni ya mwezi mzima ambayo yamkini , ikatawaliwa na mada ya uchumi. Wachunguzi wanahisi huu ni uchaguzi mgumu sana kuagua ni chama gani kitaibuka mshindi, hasa kati ya vyama vikuu, Labour cha Bw.Brown na Conservative cha David Cameron.
Akisimama pamoja na wajumbe wa Baraza lake la mawaziri nje ya Jumba lake la 10 Downing Street, huko London, hii leo, waziri-mkuu Brown alikomesha wiki kadhaa za uvumi kwa kuthibitisha Mei 6 ijayo, ni siku ya uchaguzi mkuu, kiasi cha mwezi tu kabla muda wa mwisho wa kuitisha uchaguzi.
Akitangaza tarehe hiyo, Bw. Brown alisema,
"Pengine , hii ni siri kubwa inayojulikana katika miaka ya karibuni . Malkia ameridhia kuvunjwa Bunge na kufanyika uchaguzi mkuu Mei 6."
Akianza juhudi zake kurefusha mwaka wa 13 wa kun'gan'gania chama chake cha Labour hatamu za serikali, Bw. Gordon Brown alidai kwamba serikali yake imejitahidi sana kukabiliana na msukosuko mkubwa kabisa wa kiuchumi kuzipigania familia zinazotumika kwa bidii za mapato ya wastani na ya chini kabisa . Akanadi kwamba mnamo wiki zijazo atafunga safari za kampeni kote nchini akiwa na risala moja kuu:
"Uingereza, iko njiani kufufuka kiuchumi.Tusifanye lolote ambalo litahatarisha kustawi huko kwa uchumi."
Chama cha Upinzani cha Conservative, lakini, kinaongoza mbele ya chama cha Labour katika kura ya maoni. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo wa mwezi ujao, hayako wazi, kwa vile, wananchi wanavyo ungamkono vyama vyote hivyo 2 vikuu -Labour na Conservative- ni kwa jicho la wasi wasi. Isitoshe, upinzani unakabiliwa na mtihani mkubwa katika kushika hatamu za serikali.Kwa hivyo, uchaguzi unabainisha kwamba, hakuna chama Bungeni kitakachoibuka na wingi wa kutosha ili kutawala katika kile kinachoitwa "Hung Parliament"
Kwa hivyo, matokeo yasio wazi ya uchaguzi huu ni nadra nchini Uingereza na mara ya mwisho hali kama hiyo ilitokea, ilikuwa 1974.Isitoshe, ni hali inayotisha kwa masoko ya fedha yanayopendelea matokeo wazi ya uchaguzi pamoja na ahadi thabiti ya kupambana na kasoro katika bajeti ya serikali ambayo hivi sasa, imefikia 12% ya pato zima la taifa.
Tayari hii leo, Paund ya Uingereza, imeanguka thamani yake mbele ya dala ya Marekani kwa 1% na hii, ni athari ya msukosuko wa hali ya sasa ya kisiasa.
"Sarafu ya Paund sterling, sasa itakuwa mada kubwa ya kura za maoni hadi siku ya uchaguzi Mei 6. Maoni yatakayobainisha hakuna wingi wa viti kwa chama cha Conservative, yataiumbisha Paund."-alisema Michael Hewson, mchambuzi wa soko la CMC.
Kiongozi wa Upinzani wa chama cha Conservative, David Cameron, akiwahutubia wafuasi wake ukingoni mwa Mto Thames, upande wa pili wa Bunge la Uingereza, aliueleza uchaguzi ujao kuwa, ndio uchaguzi muhimu sana tangu enzi nyingi zilizopita.
Mwito wake alioutoa ni huu :" Hampasi kuvumilia miaka 5 mengine ya Gordon Brown."
Jinsi gani ya kuongoza sasa uchumi wa Uingereza, unaofufuka kutoka msukosuko mkubwa ulioikumba nchi hii tangu vita vya pili vya dunia, yamkini ikawa mada kuu katika kamapeni ilioanza ya uchaguzi hadi Mei 6.
Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE
Uhariri: Miraji Othman