Waziri mkuu ajiuzulu Sri-Lanka
9 Mei 2022Waziri Mkuu wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa hatimae amejiuzulu leo Jumatatu kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya umma ya kumtaka yeye na kakaake ambaye ni rais wa nchi hiyo wajiuzulu kufuatia hali mbaya ya mgogoro wa kiuchumi.
Hali mbaya ya mgogoro wa kiuchumi ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa miongo nchini humo ndiyo iliyozusha maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Sri Lanka kwa wiki kadhaa. Tayari watu wawili akiwemo mbunge wa chama tawala wameuwawa na watu 139 wamejeruhiwa katika vurugu zilizozuka hii leo.
Msaidizi wa waziri mkuu, Wijayananda Herath amethibitisha kwamba Mahinda Rajapaksta amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais Gotabaya Rajapaksa. Hakuna tamko jingine rasmi lililotolewa kutoka ofisi ya rais la kuthibitisha ripoti hiyo.
Lakini kujiuzulu huku kwa waziri mkuu kumefanyika baada ya mamlaka kupeleka wanajeshi katika mji mkuu Colombo kufuatia tukio la wafuasi wa serikali mapema hii leo kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi nje ya ofisi za rais na waziri mkuu.
Vyama vya wafanyabiashara pia navyo viliitisha mgomo wa nchi nzima leo Jumatatu utakaoendelea mpaka rais na watu wengine wote wa familia yake walioko madarakani watakapoondoka. Sri Lanka nchi ya kisiwa cha Bahari ya Hindi iko ukingoni kabisa kutumbukia katika hali ya Muflisi na imesimamisha hatua zote za kufanya malipo ya mikopo inayodaiwa nje.
Nchi hiyo ilikuwa ikisubiriwa ilipe dola bilioni 7 za mkopo iliyochukua kutoka taasisi za fedha za kigeni mwaka huu kati ya bilioni 25 inazopaswa kulipa kufikia mwaka 2026. Matatizo yake ya kiuchumi yamechochea mgogoro wa kisiasa ambapo serikali inakabiliwa na maandamano yaliyoenea nchi nzima na muswaada wa kutokuwa na imani na serikali ukifikishwa bungeni.
Na hivi sasa kujiuzulu kwa waziri mkuu kunamaanisha kwamba baraza zima la mawaziri limevunjwa. Wafuasi wa waziri mkuu Mahinda Rajapaksa walikusanyika nje ya ofisi yake asubuhi ya leo wakimtaka apuuze shinikizo la waandamanaji la kumtaka ajiuzulu. Na kituo cha Televisheni cha Sirasa kiliwaonesha wafuasi hao wakiwashambulia waandamanaji kwa marungu na vyuma, pamoja na kuvunja na kuyatia moto mahema yao. Na jeshi lilipelekwa katika mji mkuu, Colombo wakati waandamanaji kwa upande wmingine wakiwashutumu polisi kwa kushindwa kuzuia mashambulizi dhidi yao.
Kwa mujibu wa afisa mmoja ambaye hakutaja jina, watu 23 wamepelekwa hospitali wakiwa na majeraha mabaya. Ni siku ya 31 ya maandamano yanayoitikisa nchi hiyo, ya kumtaka waziri mkuu, rais na wanafamilia wengine wa ukoo wa Rajapaksa wanaoshikilia madaraka makubwa serikali kujiuzulu. Tayari wabunge watatu kati ya watano wa familia ya Rajapaksa walijiuzulu kwenye nafasi walizokuwa nazo kwenye baraza la mawaziri mnamo mwezi Aprili.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Grace Patricia Kabogo