1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu Abe aitembelea Pearl Harbor

Sylvia Mwehozi
27 Desemba 2016

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ameweka shada la maua kwenye makaburi na sehemu za kumbukumbu vilivyoko Hawaii kisiwani Oahu huku akimtarajia Rais Barack Obama wa Marekani katika ziara ya kihistoria ya Pearl Harbour.

https://p.dw.com/p/2UvUH
USA Abe gedenkt als erster japanischer Regierungschef der Opfer von Pearl Harbor
Picha: picture alliance/Kyodo

Viongozi hao wawili watatembelea kituo cha manowari ya kivita kisiwani humo ambako mwaka 1941 uvamizi wa Japan uliipelekea Marekani katika vita ya pili ya dunia. Abe aliyewasili jana Hawaii, alitembelea makuburi ya kumbukumbu ya kitaifa ya Pasifiki na kuweka shada ya maua. Shinzo Abe amesema "chini ya muungano wa matumaini, ninavyoweza kuuita, ninaamini kwamba Japan na Marekani zitafanya kazi pamoja kuelezea changamoto kadhaa sio tu za kikanda bali pia za kimataifa".

Ziara hiyo ya baada ya miaka 75 tangu Japani ilipofanya mashambulizi ya kushtukiza inalenga kuonyesha mahusiano baina ya nchi hizo mbili na ziara ya rais Obama mwezi Mei katika eneo la Hiroshima ambako Marekani ilidondosha bomu la kwanza la atomiki.

Japan Hiroschima Obama Kranzniederlegung Gedenkstätte
Rais Barack Obama na waziri mkuu Shinzo Abe walipozuru Hiroshima mwezi MeiPicha: Getty Images/AFP/J. Eisele

Manowari ya kivita

Viongozi hao watazuru mabaki ya manowari ya kivita ya USS Arizona ambamo mabaharia 1,177 pamoja na wanamaji walikufa. Mabaki ya manowari hiyo bado yanaonekana mpaka leo.  Kwa mujibu wa maafisa wa seikali wa Japan, waziri mkuu Abe hatoomba radhi kwa shambulizi la Desemba 7 mwaka 1941. Shambulizi hilo liliwaua wamarekani 2403.

China hata hivyo imeikosoa ziara ya waziri mkuu Abe ikiita ni "ishara ya kujidai", na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Japan, Hua Chunying anasema bila ya kuwepo na maridhiano ya amani na China na wahanga wengine barani Asia, Japan haiwezi kuacha historia hiyo nyuma.

Umuhimu wa maridhiano

Kiongozi huyo wa Japan anayo matumaini makubwa katika ziara hiyo na rais Obama kwasababu anaamini kuna umuhimu wa kufanya maridhiano na kuwaombea wote waliouawa katika vita. 

Pearl Harbor
Picha ya juu ikionyesha kituo cha kijeshi cha majini Pearl HarborPicha: public domain/USN

Ingawa ziara hiyo haitakuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Japan, itakuwa ni ziara muhimu, kwasabau waziri mkuu Abe anasimama sambamba na rais wa sasa wa Marekani kuwakumbuka waliouawa katika vita baina ya mataifa hayo mawili.

Mwezi Mei, Obama alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea Hiroshima, ambako vikosi vya nchi hiyo viliangusha bomu la nyuklia mwishoni mwa vita. Obama hakuomba radhi kwa matendo yaliyofanywa na Marekani lakini alizungumzia umuhimu wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia.

Obama na Abe watafanya mkutano wa pamoja kabla ya kuitembelea manowari ya kivita ya USS Arizona pamoja na kuwahutubia hadhara ya wamarekani, wakazi wa hapo na maafisa wa kijeshi wakiwemo wakongwe na manusura wa shambulio hilo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef