Waziri Clinton aitembelea China
19 Februari 2009Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton anatarajiwa kuitembelea Jamhuri ya Umma wa China, kituo chake cha mwisho cha ziara yake barani Asia. Vyombo vya habari vya China vinaripoti kuhusu wazo lake la utawala nadhifu na kutarajia mambo mapya katika sera za Marekani. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yana matumaini Bi Clinton atatumia ujasiri wake kuzungumzia maswala tete yasiyoipendeza China.
Jina la Hillary Clinton linajulikana sana nchini China. Wachina wengi wanamfahamu kama mke wa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton. Juhudi zake za kugombea uteuzi wa chama cha Democratic kugombea urais wa Marekani zilifuatiliwa kwa karibu na wengi. wazo lake la utawala nadhifu liliripotiwa sana na vyombo vingi vya habari vya China.
Sasa akiwa katika ziara yake ya kwanza kama waziri wa kigeni wa Marekani Bi Clinton anatarajiwa kuitembelea China.
Kitamaduni mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani wamekuwa wakizitembelea nchi washirika. Profesa Wang Feiling wa shule ya Sam Nunn inayofunza maswala ya kimataifa katika taasisi ya teknolojia ya Georgia anaamini utawala wa Obama kutumia ziara ya waziri Clinton barani Asia, unataka kuashiria kitu.
"Hii inaonyesha kwamba utawala wa rais Obama unaupa umuhimu mkubwa uhusiano na nchi za Asia. Kwa upande mwingine inaweza kufahamika kuwa rais Obama anataka kuleta usawa katika sera za kigeni za Marekani. Bila shaka Asia ina jukumu kubwa katika siasa za ulimwengu."
Kabla kuanza ziara yake, Clinton alitoa hotuba yake ya kwanza kuhusu sera za kigeni mbele ya jarida la Asia Society mjini New York Marekani Ijumaa wiki iliyopita. Alisisitiza kuwa wakati huu wa mgogoro wa kiuchumi na kuporomoka kwa masoko ya fedha anataka kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na China. Maswala mengine ni ulinzi wa mazingira, uvumbuzi wa nishati inayoweza kutengenezwa upya, usafirishaji wa teknolojia pamoja na vita dhidi ya maharamia katika eneo la pembe ya Afrika.
Kuhusiana na swala la Korea Kaskazini Bi Clinton ameeleza wazi kwamba Marekani inahitaji ushirikiano na msaada wa China. Pia amezungumzia kuwa na uhusiano mzuri na China licha ya kutofautiana.
Katika ziara ya waziri Clinton nchini China, profesa Li Cheng, mtafiti mkuu wa taasisi ya Brooking na mtaalam wa uhusiano kati ya Marekani na China anaona uwezekano wa mabadiliko katika sera ya kigeni ya Marekani iliyowatambua marafiki na maadui.
"China ni mshirika muhimu wa Marekani kwa kila upande. Clinton pia amesema China si adui wa Marekani. Nchi hizi ni injini mbili kubwa za uchumi wa dunia. Ukitaza nyuma kuna mgogoro wa kiuchumi, lakini mbele kuna ushirikiano kati ya China na Marekani. Ni kwa njia hii pekee nchi hizi zitaweza kukabiliana na mgogoro huu na kufufua biashara ya kimataifa. Pia katika maswala ya kijeshi kuna uwezekano mkubwa wa ushirikiano. Kuna jambo moja tu ambalo Marekani na China hazitakubaliana; haki za binadamu hususan swala la Tibet."
Mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu yakiwemo Amnesty International, International Campaign for Tibet na Waandishi habari wasio mipaka, yamemtaka Hillary Clinton azungumzie hali ya haki za binadamu na swala la jimbo la Tibet pamoja na viongozi wa China.
Liao Tianqai anafanya kazi na wakfu wa utafiti wa Laogai mjini Washington ambao kwa miaka mingi umekuwa ukijishughulisha na haki za binadamu nchini China. Liao ana matumaini makubwa na ziara ya Clinton nchini humo.
"Clinton mara hii nchini China atazungumzia swala la haki za binadamu. Alipoitembelea China mwaka 1995 kama mke wa rais, alizungumzia haki za wanawake. Binafsi ningependa sana kuona kama Clinton ataweza kugusia ukandamizaji wa watetezi wa haki za binadamu na wakosoaji wa serikali. Kama mwanamke Bi Clinton anatakiwa kuzungumzia sera ya China ya kuzaa mtoto mmoja. Sera hii imesababisha uchungu miongoni mwa wanawake wengi na lazima ifikiriwe upya."
Orodha ya matarajio ya Wachina kwa Bi Hillary Clinton ni ndefu. Ikiwa kweli kiongozi huyo atayazungumzia maswala haya na viongozi wenzake wa China, ni jambo la kusubiri na kuona. Clinton atalazimika kudhihirisha katika ziara yake jinsi anavyojua kutumia maarifa kuleta utawala nadhifu nchini China.