Wazimbabwe wasusia kazi na kubakia makwao
6 Julai 2016Siku hiyo ya kususia kazi iliyoitishwa na kuongozwa na vuguvugu la kwenye mtandao wa kijamii linaloitwa "This flag", inajiri baada ya kushuhudiwa makabiliano makali baina ya madereva wa teksi na polisi Jumatatu yaliyopelekea kukamatwa kwa watu 95.
Haya yanafanyika wakati ambapo kuna mgomo wa walimu, wahudumu wa afya pamoja na madakatari kutokana na kucheleweshwa kwa mishahara yao.
Taifa hilo la kusini mwa Afrika limekumbwa na hali mbaya ya ukame, iliyochochea zaidi tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na uhaba mkubwa wa fedha uliowaghadhabisha raia wake. "This flag" ni vuguvugu lililoanzishwa mwezi Aprili na muhubiri mmoja wa kikristo Evan Mawarire kuipinga serikali kwa kufumbia macho ufisadi, ukosefu wa haki na umasikini.
"Wakati wa kusema basi'
Kampeni hiyo imewavutia maelfu ya wafuasi, ambao wamekuwa wakizungumzia dhidi ya ubadhirifu wa serikali. Harakati hiyo ya kujitenga na kufanya kazi iliandaliwa kupitia mitandao ya kijamii ya twitter, facebook na whatsapp.
"Tumefikia wakati sasa ambapo kila mmoja anasema ni basi. Watu wamejitokeza kwa wingi, hili ndilo tulilokuwa tunataka, kitu ambacho sote tunaweza kukifanya kwa pamoja," alisema Mawarire alipoulizwa kuhusiana na ufanisi uliopata hatua hiyo ya kutokwenda kazini.
Shirika la kitaifa linalodhibiti mawasiliano Zimbabwe POTRAZ katika taarifa limesema kwamba litawakamata wale wote wanaotuma jumbe zitakazopelekea kuzua fujo.
Vyombo vya habari vya kibinafsi nchini zimbabwe vimeripoti kwamba raia wa nchi hiyo katika miji mingine mikubwa walisalia nyumbani pia, huku biashara nyingi zikifungwa. Mara ya mwisho Zimbabwe kushuhudia raia kususia kwenda kazini ilikuwa Aprili mwaka 2007.
Wakati huo huo shirika la habari la AP limeripoti kwamba mtandao wa intaneti ulizimwa kwa kipindi kikubwa cha jumatano na huduma zilikuwa pole pole ziliporejea. Polisi wanaripotiwa pia kuwazuilia wanahabari kadhaa na kuwashurutisha kufuta picha za makabiliano baina ya polisi na wakaazi wa Harare.
Vitendo vya kuwapinga polisi na kukabiliana nao si rahisi kutokea nchini Zimbabwe ingawa katika wiki chache zilizopita pingamizi zimezidi kufuatia ugumu wa maisha na madai ya ubadhirifu wa serikali.
Kucheleweshwa mishahara
Serikali ya rais Robert Mugabe imechelewesha malipo ya wafanyakazi wa umma kufuatia upungufu wa fedha katika hazina kuu ya serikali baada ya miaka kadhaa ya kudorora kwa uchumi na kiangazi kilicholemaza kilimo.
Kwa mujibu wa maafisa Zimbabwe inatumia yamkini asilimia 80 ya pato lake kwa malipo ya wafanyakazi wa umma, huku ikiwa asilimia 90 ya idadi ya watu wakiwa hawana ajira rasmi.
Mitaa ya mji wa Harare ambayo kwa kawaida hushuhudia shughuli chungunzima, ilikuwa mitupu kufuatia mgomo huo ulioitishwa na mashirika ya kijamii ili kumshinikiza rais Mugabe kukabiliana na mzozo huo wa kiuchumi.
"Siwezi kwenda kazini wakati nchi nzima haiendi," alisema Sybert Marumo, anayefanya kazi katika duka la vifaa vya kielektroniki. "Maisha ni magumu na tunastahili kuionyesha serikali kwamba tumefika ukingoni."
Wanafunzi wameonekana wakirudi nyumbani baada ya walimu wao kukosa kufika shuleni. Katika mji wa kusini mashariki wa Masvingo polisi waliwatawanya waandamanaji walioziba njia kwa kuchoma magurudumu.
Mgomo huu ndio wa hivi majuzi dhidi ya serikali ya rais Mugabe ukimtaka kiongozi huyo aliye uongozini tangu mwaka 1980 kuachia ngazi.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AP/AFP
Mhariri:Idd Ssessanga