Wazee Tanzania wairai serikali mauaji ya vikongwe
1 Oktoba 2018Macho na masikio ya wazee wengi nchini Tanzania katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani mwaka huu yalikuwa kusikia tamko la serikali kuhusu lini sheria ya kusimamia mustakabali wa maisha ya wazee itatungwa pamoja na kupewa pensheni itakayosaidia kupunguza makali ya maisha kutokana na wengi kuishi katika lindi la umasikini.
Wazee wanalalamika kuwa mazingira wanamoishi kwa sasa ni ya hatari na yamewafanya wengi kupoteza maisha kabla hata ya kulemewa na uzee wao, wapo wanaouawa kwa imani za kishirikina na baadhi kutelekezwa na familia zao na kujikuta wakikosa mahitaji na baadaye kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa takwimu za wazee nchini Tanzania asilimia ishirini na saba ya wazee wote laki sita sabini na saba na arobaini na tatu wanaishi wenyewe bila msaada wa mtu yeyote huku asilimia themanini na tatu wakiishi katika familia.
Rais msaafu wa Tanzania Alhaj Alli Hassan Mwinyi mgeni rasmi katika maaadhimisho hayo alizitaka mamlaka za maamuzi likiwemo bunge na baraza la mawaziri kuhakikisha wanafanyia maamuzi masuala ya maslahi ya wazee nchini Tanzania.
Shirika la Dorcas Aid International Tanzania ni moja kati ya mashirika yanayosaidia wazee wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na hali zao mbalimbali. Afisa miradi wa shirika hilo Joseph Kumwembe anasema wazee wanakabiliwa na hali ngumu na kutaka wadau mbalimbali ikiwemo jamii kujitokeza kuokoa maisha ya wazee.
Waziri wa Afya nchini Tanzania Umi Mwalimu akizungumza katika maadhimisho hayo ametoa wito kwa wahudumu wa afya nchini Tanzania kutoa huduma bora na Rafiki kwa wazee na kuonya kuwa watakaokwenda kinyume na agizo hilo watachukukuliwa hatua za kisheria.
Nchini Tanzania kuna wazee milioni mbili na wanaopata pensheni ni asilimia nne na kundi kubwa la asilimia tisini na sita wakiwa hawana kipato na wengi wanaishi kwa kutegemea familia zao na wahisani mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Mwandishi: Charles Ngereza, DW-Arusha
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman