1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili wauawa kwenye maandamano Kongo

31 Desemba 2017

 Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema maafisa wa usalama wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamewaua watu wawili kwa kuwapiga risasi wakati wa maandamano ya kumpinga rais Joseph Kabila.

https://p.dw.com/p/2qALX
Kongo Kinshasa Unruhen wegen Präsident Kabila
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Mkurugenzi wa Afrika ya Kati wa Human Rights Watch Ida Sawyer amesema watu hao wameuliwa nje ya kanisa la Mtakatifu Alphonse katika wilaya ya Matete katika jiji la Kinshasa. Msemaji wa polisi Pierrot Mwanamputu hata hivyo amekanusha kwamba polisi walitumia risasi wakati wa maandamano hayo.

Watu kadhaa walijeruhiwa wakati vikosi vya usalama nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vilipoyavunja maandamano hayo yaliyofanyika Jumapili Tarehe 31.12.2017 ya kumpinga Rais Joseph Kabila. Inadaiwa kuwa afisa mmoja wa usalama alitishia kuwapiga risasi waandishi wa habari wa shirika la AFP waliokuwa wanafuatilia maandamano hayo mjini Kinshasa.

Shrika la habari la AFP limeripoti kwamba watu wapatao 10 walijeruhiwa, miongoni mwao ni padri aliyeumia usoni huku mwanamke mmoja aliye na umri wa miaka sitini alifura nundu kwenye paji la uso wake, baada ya polisi kutumia nguvu wakati wa kuvunja mikusanyiko ya watu ndani ya makanisa katikati ya mji wa Kinshasa.

Waandamanaji wanataka Kabila atoe ahadi kuwa hatawania muhula wa tatu wa uongozi. Rais Kabila amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 aliposhika madaraka ya urais baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa.

Rais wa DRC Joseph Kabila
Rais wa DRC Joseph KabilaPicha: Imago/Xinhua

Rais Kabila alikataa kujiuzulu baada ya kumalizika kipindi chake cha pili na cha mwisho mnamo Desemba 2016 na tangu hapo uchaguzi wa urais umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara na sasa umepangiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao wa 2018.

Maafisa wa usalama wamewakamata watumishi 12 wa madhabahu wa Kanisa Katoliki waliokuwa  wakiongoza upinzani dhidi ya rais Kabila nje ya Kanisa. Kanisa Katoliki lilikuwa limetoa wito wa kufanyika maandamano ya amani siku ya Jumapili, ambayo yaliungwa mkono na vyama vikubwa vya upinzani pamoja na makundi ya kiraia.

Polisi wapambana na wanaoandamana dhidi ya Kabila
Polisi wapambana na wanaoandamana dhidi ya rais KabilaPicha: picture alliance/AP Photo/J. Bompengo

Serikali kwa upande wake iliweka vikosi vya usalama kote katika jiji la Kinshasa lenye watu milioni 10 na watu wengi wameliambia shirika ka habari la AFP kwamba vikosi vya usalama vilitumia nguvu dhidi ya waandamanaji waliokuwa kwenye makanisa. Kwa mujibu wa shirika la AFP, mwandishi mmoja wa habari wa kituo cha redio cha Ufaransa RFI alizuiliwa na polisi kwa muda mfupi.

Serikali ilikataa kutoa vibali kwa ajili ya maandamano hayo ya Jumapili, na ilifunga huduma za mitandao ya kijamii pamoja na huduma za ujumbe mfupi kabla ya maandamano hayo kuanza katika kile serikali inachokiita kuwa ni sababu za kiusalama.

Waumini wakiwa Kanisani
Waumini wakiwa KanisaniPicha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Makanisa zaidi ya 160 yalishiriki katika maandamano hayo ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi katika baadhi ya sehemu za jiji la Kinshasa. Maandamano yamekuwa yakipigwa marufuku licha ya wakati mwingine waandamanaji kukiuka amri ya serikali na kuendelea na maandamano hali ambayo pia imekuwa ikisababisha machafuko.

Hatua ya kanisa Katoliki kuitisha maandamano ya leo Jumapili imewafanya baadhi ya wachambuzi kuonya juu ya uwezekano wa kukosekana utulivu. Jason Stearns mchambuzi aliyebobea katika masuala ya siasa za Kongo kutoka chuo kikuu cha New York kinachohusika na mahusiano ya kimataifa mapema leo aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba maandamano ya leo Jumapili nchini Kongo yangekuwa makubwa zaidi kuliko yale ya mwaka jana.

Katiba ya Kongo inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu wa uongozi lakini makubaliano yaliyofikiwa yanamruhusu kubakia madarakani hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Mwandishi Zainab Aziz/APE/ARTE/AFPE

Mhariri: Jacob Safari