Wawekezaji wa kigeni wahakikishiwa usalama wao Kenya
26 Juni 2019Mbunge huyo Charles Kanyi maarufu kama Jaguar, aliipa serikali saa 24 kuwatimua wageni walioko nchini ama yeye mwenyewe awatimue.
"Kwa hivyo mimi naomba waziri waangalie hii maneno, wahakikishe kuwa wakenya wetu wanafanya biashara bila ya kushindana na wageni kutoka nchi mbali mbali, ukiangalia vile magari yanavyouzwa hapa Wapakistan wamechukua hiyo bisahara, ukiangalia Nyamakima Wachanise wamechukua hizo biashara, ukiangalia masoko zetu, Watanzania na Waganda wamechukua hizo biashara,” alisema Jaguar.
Matamshi ya mbunge huyo wa Starehe ambaye pia ni mwanamuziki Charles Kanyi yamewaacha wakenya wengi vinywa wazi. Matamshi hayo yamelaaniwa na serikali kupitia kwa msemaji wake Cyrus Oguna.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, serikali imepinga matamshi hayo na kusema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya mbunge huyo, bila ya kutaja ni hatua zipi. Kwenye video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Jaguar aliwaambia raia wa kigeni kufunga virago na kurejea kwao, na wasipofanya hivyo, atawalazimisha kuhama.
"Mimi naipa serikali saa 24, kama hao watu hawatakuwa wamerudi kwao, tutaingia kwa hayo maduka wanayofanyia kazi na kuwatoa, tutawapiga na kuwapeleka katika uwanja wa ndege,” aliendelea kusema mbunge huyo katika vidio iliyosambaa kote katika mitandao ya kijamii.
Serikali ya Kenya yajitenga na Matamshi ya mbunge Jaguar
Serikali imezidi kujitenga na matamshi hayo kwenye taarifa yake, imesema kuwa hayana nafasi katika mazingira ya watu wastaarabu kama wakenya wananoishi kwa amani na kupenda wageni wa mataifa mbali mbali. Mapema juma lililopita serikali iliwafurusha raia saba wa China kwa kuendesha ujasiriamali katika soko kubwa la Gikomba bila ya kuwa na vibali halali vya kuwa nchini.
Waziri wa usalama wa Kitaifa Fred Matiangi amesema serikali ilisitisha kuwapa vibali vya kazi wajasiriamali wote. Yeyote anayetaka kibali cha kazi atatuma maombi akiwa nchini mwake, atafika tu Kenya, akiwa na kibali hicho. amesisitiza kuwa serikali haiwapi wafanyibiashara vibali vya kazi.”
Serikali ya Tanzania ilimtaka balozi wa Kenya nchini humo kueielezea kuhusu matamshi hayo ambayo yamelaaniwa na wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii. Matamshi ya mbunge huyo yanakwenda kinyume na moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaohimiza ushirikiano kati ya raia wa mataifa husika.
Chanzo: Dw, Nairobi