1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawakilishi wa Rwanda, Kongo wakutana

27 Julai 2023

Kikao cha mazungumzo kati ya mji wa Rubavu wa Rwanda na Goma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimefanyika mjini Rubavu kukabiliana na udhalilishaji unaohusishwa na matukio ya kisiasa kati ya mataifa hayo jirani.

https://p.dw.com/p/4UTyj
Demokratische Republik Kongo | Hilfsprojekt für Frauen
Picha: Paul Lorgerie/DW

Zaidi ya miongo mitatu tangu kuzuka tena kwa migogoro na mivutano ya kikabila na kisiasa ambayo imevuruga uhusiano wa kijamii kati ya Rwanda na jirani yake, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wawakilishi wa kijamii na wafanyabiashara wamekutana kutoka miji ya Rubavu na Goma kujadiliana njia za kupambana na athari za mizozo iliyopo upande wa mashariki mwa Kongo.

Soma zaidi: Unyanyasaji wa kingono waongezeka mjini Goma, DRC

Serge Bisimwa, mratibu wa kampuni ya Benevolencia Grands Lacs iliyoandaa mikutano hii, aliiambia DW kwamba matokeo ya uhasama wa kisiasa baina ya nchi zao yanaendelea kuathiri idadi kubwa ya watu.

"Kuibuka tena kwa kundi la waasi wa M23 kumezidisha hali hiyo. Suala la vita mashariki mwa Kongo linapaswa kuachwa kwa wanasiasa wa nchi hizi mbili." Alisema Bisimwa.

Umuhimu wa kuhubiri amani

Ngoma King wa shirika la kiraia la Rwanda lililowakilishwa katika mikutano hii alisema njia pekee ya kuondokana na mgogoro wa kijamii kati ya nchi hizo mbili zinazopakana ni kuwepo kwa amani na hotuba za kuhubiri amani na upendo.

Demokratische Republik Kongo | Hilfsprojekt für Frauen
Wanawake wa Kongo wakiwa kwenye miradi ya kujiendeleza.Picha: Paul Lorgerie/DW

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na kupitishwa kwa kauli moja na washiriki wa mkutano huu ni kujitolea kuhubiri amani na kuishi pamoja.

Soma zaidi: Maporomoko ya ardhi yaua watu 10, DRC

Juhudi nyingi zinafanywa kati ya Kongo na Rwanda kuwaleta watu wa nchi hizo mbili kuishi kwa pamoja, huku kwa Wakongo wengine wakithibitisha kuwa kurejea katika kuishi pamoja kwa amani ni jambo lisilowezekana maadamu uasi wa M23 unaendelea kupamba moto nchini humo.

Mara nyingi Kinshasa inaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono M23 tuhuma ambazo zinakanushwa na Kigali. 

Imeandaliwa na Ruth Alonga/DW Goma