1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waturuki hawamtaki waziri mkuu Erdogan

3 Juni 2013

Maandamano nchini Uturuki, kadhia ya ndege zisizokuwa na rubani na madhara yake na ahadi za uchaguzi za chama cha CDU ni miongoni mwa mada zilizopewa umbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/18irP
Polisi wanafyetzua gesi za kutoa machozi katika maandamano mjini IstanbulPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini Uturuki ambako maandamano ya umma yaliyoanza wiki iliyopita yakiwa na lengo la kupinga mpango wa serikali ya waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan wa kujenga majumba katika uwanja unaotumika kama bustani ya umma,yamechukua sura ya malalamiko ya umma dhidi ya serikali hiyo,huku sauti zikipazwa kumtaka waziri mkuu ajiuzulu.Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika:"Waturuki wamesimama kidete dhidi ya "mwinyi" anaehisi anaweza kuigeuza nchi hiyo atakavyo yeye.Erdogan amesahau kwamba chama chake cha AKP-japo kama kimenyakua zaidi ya asili mia 50 katika uchaguzi wa mwaka 2011,lakini,katika mfumo wa kidemokrasia,wadhifa wake ni wa muda na hajapewa madaraka kamili ya kuweza kufanya akitakacho.Hata hivyo isisahauliwe :Upande wa upinzani unaozungumzia hivi sasa kuhusu "uislam wa kifashisti" unatia chunvi.Wamefika hadi ya kuitaja amri ya kuwekewa vizuwizi biashara ya vinywaji vikali mnamo saa za usiku kuwa ni sawa na kulazimisha mtindo wa kimaisha wa kiislam.Kimoja tu kinabidi kisemwe:tangu miaka mitatu sasa marufuku kama hayo yanaheshimiwa katika jimbo la Ujerumani la Baden-Württenberg."

Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linasema yanayotokea Uturuki,yanastahiki kufuatiliziwa kwa makini na nchi za magharibi.Gazeti linaendelea kuandika:"Lawama hazijalengwa pekee dhidi ya ujenzi wa majumba katika bustani,bali zaidi dhidi ya utawala wa kimabavu wa Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha kihafidhina cha kiislam.Hatua kali zilizochukuliwa zinabainisha wasi wasi wa serikali na mfarakano ulioko kati ya serikali na wananchi.Hali hiyo, nchi za magharibi hazistahiki kuifumbia macho.Kwasababu Uturuki,sio tu ni muhimu kutokana na nafasi yake kijeografia katika eneo la mizozo bali bia ni mshirika wao muhimu."

Thomas de Maizière atakiwa ajieleze

Kadhia ya ndege inayoruka bila ya rubani inazidi kumzonga waziri wa ulinzi Thomas de Maizière.Kila kukicha mepya yanachomoza.Gazeti la "Südwest Presse" linaandika:" Waziri wa ulinzi Thomas de Maizière yuko mashakani.Kwamba makosa katika mradi wa ndege isiyokuwa na rubani "Euro Hawk" yamegunduliwa dakika ya mwisho,ni mtihani.Utageuka kashfa lakini pindi walipa kodi wakilazimika kubeba dhamana za yaliyotokea.Kilichokwenda mwamba si suala la mkataba bali suala la usalama wa angani.Hiyo ndio sababu kwanini hakujatolewa kibali cha ndege hizo zisizokuwa na rubani.Jumatano ijayo de Maizière atalazimika kujieleza.Haitakuwa rahisi kwake.Na akikwama,bali kitanzi kitazidi kumbana kama kiongozi wa wizara ya ulinzi .

Thomas de Maizière
Waziri wa ulinzi Thomas de MaizièrePicha: Jörg Enters/DGAP

Ahadi za kansela Merkel zatiliwa shaka

 Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu ahadi za kansela katika wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi mkuu zimepamba moto.Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linaandika:

EU Gipfel Merkel PK 15.03.2013
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

 Wajerumani watakapokwenda kupiga kura mwezi September mwaka huu,mada mbili zitakuwa na umuhimu mkubwa zaidi kwao katika kuamua nani wakumpigia kura:nazo ni mzozo wa madeni barani Ulaya na juhudi za kuania usawa katika jamii.Kansela amepania kukupigania sauti katika mada zote hizo.Ni sawa lakini pia hatari.Pale Angela Merkel anapoahidi ustawi wa jamii bila ya kutaja pesa zitatoka wapi,anaitia hatarini wakati huo huo imani ya wananchi kwake,kama kiongozi aliyedhamiria kurekebisha akiba ya nchi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman