Watunisia watunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel
10 Desemba 2015Kabla ya kukabidhiwa tuzo ya amani ya Nobeli mwenyekiti wa shirika la haki za binaadam la Tunisia,Abdesattar Ben Moussa alisema tunanukuu"Silaha,kimsingi hazisaidii kitu ila maangamizi" .
Ametoa mfano wa Libya ambako anasema,watu sasa wanazungumzia kuhusu aina fulani ya mdahalo." Matatizo katika nchi jirani yanabidi yafumbuliwe kwa njia ya majadiliano pamoja na mashirika ya kiraia,vikihusishwa pia vyama vya kisiasa,wakitengwa bila ya shaka makundi ya kigaidi."
Pamoja na shirika lenye nguvu linalopigania masilahi ya wafanyakazi UGTT,jumuiya ya waajiri Utica na jumuia ya mawakili,shirika linalopigania haki za binaadam LTDH,wanaunda tume ya pande nne ya mdahalo wa taifa,waliokabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel na mwenyekiti wa kamati ya Nobel,bibi Kullmann Five.
Tume ya amani ya Nobel imeisifu Tunisia kuwa mfano wa kuigizwa katika kuipatia fumbuzi mizozo ya wakimbizi
Bibi Kullmann Five amesifu kipindi cha mpito kuelekea demokrasia nchini Tunisia akisema ni mfano mwema wa kuupatia ufumbuzi mzozo wa wakimbizi."Tunashuhudia kipindi cha misuko suko,Afrika kaskazini,Mashariki ya kati na Ulaya,mamilioni wanakimbia vita,ukandamizaji,mateso na vitisho,amesema bibi Kullmann Five. Na kuongeza:"Ingekuwa nchi zote zimefanya kama ilivyofanya Tunisia na kuandaa uwanja kwaajili ya mdahalo,uvimilivu,demokrasia na haki za binaadam,wachache tu wangelazimika kukimbia.
"Tunisia imeuonyesha ulimwengu kwamba makundi ya kidini,yakisiasa na yale yanayopigania kutenganishwa dini na siasa wanaweza kujadiliana na kupata ufumbuzi kwa masilahi ya taifa-wakiwa na nia ya kufanya hivyo.
Mwito wa kuupataiwa ufumbuzi mzozo wa Palastina
Washindi wa tuzo ya amani ya Nobel wameitumia fursa ya kukabidhiwa tuzo hiyo kutoa wito wa kuundwa dola la Palestina-ikiwa njia mojawapo wanasema ya kupambana na ugaidi.
"Tunabidi tuharakishe juhudi za kuzipatia ufumbuzi kadhia moto moto ulimwenguni na hasa kwa kulipatia ufumbuzi suala la Palestina" amesema katibu mkuu wa shirika linalotetea masilahi ya wafanyakazi UGTT Houcine Abbassi aliyeshangiriwa na kupigiwa makofi,baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo ya amani ya Nobeli mjini Oslo.
Amezungumzia umuhimu wa kuendelezwa mjadala kati ya watu wa tamaduni tofauti pamoja na kuishi kwa amani,kwa misingi ya kuheshimiana licha ya tofauti zilizoko-akitaja mapambano dhidi ya ugaidi kuwa kipa umbele kupita vyote.
Hatua za ulinzi zimeimarishwa kufuatia kitisho cha mashambulio ya kigaidi. Mbali sherehe na tuzo ya amani ya Nobel mjini Olso,zawadi nyengine za Nobeli zimetolewa hii leo mjini Stockholm; tuzo ya Nobeli ya fasihi,kemia,tiba,fizikia na uchumi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman