Marekani yajieleza kwa kutohudhuria maandamano ya mshikamano
16 Januari 2015Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry mjini Paris imelengwa kutuliza lawama zilizozosababishwa na kutohudhuria afisa wa ngazi ya juu wa Marekani katika maandamano ya wiki iliyopita ya mshikamano wa kimataifa dhidi ya mashambulio ya kigaidi yaliyoangamiza maisha ya watu 17 mjini Paris.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alizungumza kwanza na kwa muda mfupi na waziri mwenzake Laurent Fabius na kumueleza alikuwa ziarani mjini Sofia na nchini India na ndio maana hakuweza kushiriki katika maandamano ya jumapili iliyopita mjini Paris.
Ushirikiano kusaka jibu la pamoja dhidi ya ugaidi
Baadae alikaribishwa katika kasri la Elysée kwa mazungumzo pamoja na rais Francois Hollande aliemtolea wito John Kerry kwa pamoja wasake "majibu yanayohitajika" kufuatia mashambulio ya kigaidi ya wiki iliyopita nchini Ufaransa.
Baadae,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,John Kerry ,akifuatana na waziri mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius aliweka mashada 2 ya mauwa,kwanza mbele ya jengo la jarida la Charlie Hebdo na la pili katika duka la kiyahudi mjini Paris kuwakumbuka wahanga 17 wa mashambulio ya wiki iliyopita
Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani inafanyika baada ya ikulu ya Marekani kukiri imefanya kosa kwa kutomtuma mwakilishi wa ngazi ya juu badala ya balozi wake nchini Ufaransa,Jane Hartley kuhudhuria maandamano ya jumapili iliyopita.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji,Didier Reynders amesema opereshini ya kuwaandama watuhumiwa wa kigaidi katika mji wa Verviers,imemalizika.Watuhumiwa wawili wa kigaidi waliokuwa wakiandaa mashambulio dhidi ya nchi hiyo ya kifalme wameuliwa."Polisi ya Ubeligiji imesema mtu wa tatu anaetuhumiwa kushirikiana na watuhumiwa hao wawili wa kigaidi amekamatwa katika mji huo wa karibu na mpaka wa Ujerumani.
Nchini Ujerumani pia watuhumiwa wawili wamekamatwa kwa madai ya kushirikiana na wafuasi wa itikadi kali mjini Berlin.
Toleo jipya la Charlie Hebdo lakosolewa na nchi za kiislam
Katika wakati ambapo msako dhidi ya watuhumiwa wa kigaidi unaendelea nchini Ufaransa,Ubeligiji na Ujerumani,toleo jipya la jarida la Charlie Hebdo limekosolewa na kuzusha wimbi la maandamano katika nchi tofauti za kiislam.Maandamano dhidi ya toleo hilo jipya lililochapishwa kwa zaidi ya nakala milioni tano linalotajwa kuwa ni tusi kwa waumini bilioni mbili wa dini ya kiislam ulimwenguni yanatazamiwa kufanyika pia baada ya sala ya ijumaa hii leo katika nchi hizo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/
Mhariri:Yusuf Saumu