Watu zaidi ya 50 wafa kwa kukosa hewa, wakati wakisafirishwa kutoka Myanmar kuelekea Thailand kwa njia haramu.
10 Aprili 2008Wahamiaji hao 56 wa Myanmar waliokufa, na wengine 21 ambao wako hospitali, walikumbwa na mauti hayo mpakani mwa nchi hizo mbili kutokana na kukosa kuvuta hewa safi, wakati walipokuwa wakisafirishwa isivyo halali, ndani ya kontena hilo ambalo kawaida hutumika kuhifadhia vyakula baridi vya baharini.
Afisa wa polisi katika jimbo la magharibi mwa pwani ya Thailand la Ranong, Phuvanai Wattanasamai amesema wahanga hao ni miongoni mwa watu 121 waliokuwa wamejazana ndani ya kontena hiyo, iliyokuwa na urefu wa mita sita na upana wa mita 2.2 tu na kwamba watu hao 21 ambao walikuwa katika hali mbaya walikimbizwa hospitali kwa matibabu na kwamba wengine wanahojiwa na polisi.
Anasema watu hao waliwekwa ndani ya kontena katika lori hilo, lililokuwa limefungwa kabisa kwa saa kadhaa bila ya hewa, kutokana na kwamba kiyoyozi kilichokuwa kinatumika kutolea hewa kushindwa kufanya kazi na kwamba wengi walikuwa wakipiga kontena hilo kwa nguvu kwa nia ya kuomba msaada.
Baada ya watu hao kupiga kelele kwa muda mrefu, Dereva alilipaki lori hilo, pembeni kwa nia ya kuwezesha watu hao kutoka na kwamba akakimbia baada ya kuona nusu ya abira wake wamekufa.
Miili hiyo iligunduliwa katika jimbo hilo la kusini lililo mpakani la Ranong, baada ya polisi kukuta lori hilo, ambalo wahamiaji hao haramu walikuwa wamejificha wakijaribu kuingia Thailand kwa nia ya kwenda kufanya kazi likiwa limetelekezwa.
Watu walionusurika katika tukio hilo wamearifu kuwa walikuwa wakipiga kelele kumwambia dereva huyo kwamba wanakufa kutokana na kukosa hewa, lakini aliwajibu kwamba wanyamaze kwani wangesikiwa na polisi wakati walipokuwa wakivuka kizuizi.
walikuwa wakitokea katika kisiwa cha Viktoria wakielekea Phuket na majimbo mengine ya Thailand kwa ajili ya kutafuta kazi na kwamba walikuwa wakiwasiliana na dereva huyo kwa njia ya simu ya mkononi kumfahamisha kuhusiana na joto pamoja na kukosa hewa ndani ya kontena hilo.
Afisa Mwandamizi wa jeshi la polisi katika jimbo hilo amefahamisha kuwa kati ya hao waliokufa 37 walikuwa ni wanawake na kweamba polisi wanawashikilia watu wengine 37 waliookoka kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Amesema wanataka kujua kwamba wahamiaji hao ni sehemu ya mtandao wa biashara haramu katika eneo hilo.
Zaidi ya watu milioni moja kutoka Myanmar , Laos na Cambodia wanakadiriwa kufanya kazi nchini Thailand ambapo wengi wao wanafanyakazi kinyume cha sheria katika viwanda, mahoteli na kazi nyingine zikiwemo za nyumbani.
Wanapoingia nchini Thailand mara nyingi hujificha chini ya bidhaa mbalimbali kama vile matunda na mboga za majani zilizopakiwa katika malori makubwa ama madogo ya mizigo.
Katika kipindi cha mwaka uliopita wafanyakazi 11 wa
Myanmar walikufa baada ya gari lililokuwa limepakiza kupata ajali karibu na mpaka wa nchi hiyo na Thailand.