Watu zaidi ya 400 wamenyongwa Iran mwaka huu
3 Septemba 2024Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko la unyongaji watu nchini Iran mwezi uliopita lililoifikisha idadi jumla ya watu walionyongwa kufikia zaidi ya 400.
Kundi la wataalumu huru 11 wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema katika taarifa yao kwamba watu wasiopungua 81 walinyongwa nchini Iran mnamo mwezi Agosti pekee, ikiwa ni zaidi ya 45 ya wale walionyongwa mwezi Julai.
Wataalamu hao wamesema idadi ya watu walionyongwa tangu mwanzo wa mwaka 2024 imeongezeka kupita 400 wakiwemo wanawake 15.
Wataalamu hao wanaoteuliwa na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lakini hawazungumzi kwa niaba ya umoja huo, wamesema wametiwa wasiwasi sana na ongezeko hilo kubwa la watu kunyongwa.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, likiwemo Amnesty International, Iran huwanyonga watu wengi zaidi kila mwaka kuliko nchi yoyote nyingine duniani isipokuwa China.