1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia

Abdu Said Mtullya11 Februari 2010

Mapambano yamepamba moto nchini Somalia ,watu zaidi ya 30 wamekufa na mamia wanayakimbia mapigano mjini Mogadishu.

https://p.dw.com/p/Lyff
Wapiganaji wa al-Shabaab.wanaodhamiria kuiangusha serikali ya mpito nchini Somalia.Picha: AP

Watu wasiopungua 30   wameuawa mjini Mogadishu kutokana na mapambano   baina ya majeshi ya serikali na  wapinzani wa kiislamu.

Maafisa wa serikali pia wamearifu kwamba watu   wengine zaidi ya  60 wamejeruhiwa katika  mapambano hayo yaliyopamba moto tokea jana.

Wanajeshi wa serikali ya  Somalia walitumia mizinga kuzishambulia sehemu  za wapinzani katika soko la  Bakara-  sehemu ambapo  watu  wengi wanaishi.

Majeshi ya serikali yalichukua   hatua baada ya kushambuliwa na wapinzani hapo jana.

Habari zinasema watu wasiopungua 30 wameuawa  tokea jana na wengine zaidi  ya 60 wamejeruhiwa katika  mapigano hayo.

Daktari mmoja kwenye  hospitali ya Madina mjini Mogadishu amesema hospitali yao imepokea majeruhi 61. Daktari huyo aliliambia shirika    la habari la Ujerumani dpa kuwa watu watatu walikufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini.Watu  hao walikufa wakati    walipokuwa wanatibiwa.

Kundi la wapinzani  al-Shabaab ambalo hivi karibuni lilitangaza    kujiunga na mtanda wa al-qaida limepania kuing'oa  serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za magharibi. Wapinzani hao  wanaidhibiti sehemu kubwa    ya mji mkuu- Mogadishu pamoja na sehemu za kusini  na za kati nchini Somalia.

Radio Shabelle imeripoti kwamba sehemu kadha za mji   wa Mogadishu zimeshambuliwa kwa makombora, na mamia ya   raia wanayakimbia mapigano hayo baina ya majeshi ya serikali na wapinzani wa al-Shabaab. Msemaji wa kitengo  cha misaada amelalamika   kwamba majeshi ya serikali na wapiganaji wa  al-Shabaab   wameweka vizuizi vinavyozuia kutolewa kwa huduma  za haraka  kwa majeruhi  ambao  wangeliweza kupelekwa   haraka kwenye hospitali  ambazo bado zinafanya kazi  mjini Mogadishu.

 Msemaji huyo  amezitaka pande zinazopigana    ziyaruhusu magari  ya kuwahudumia wagonjwa yapite.

Katika siku za hivi karibuni mamia ya wapiganaji wa   al-Shabaab wamekuwa wanamiminikia katika  mji wa Mogadishu.

Serikali ya mpito  nchini   Somalia inayoongozwa  na rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed  mwenye mtazamo wa  ukadirifu inategemea msaada wa wanajeshi wapatao 5200  wa  Umoja wa Afrika.

Hatahivyo wanajeshi hao  wanalinda usalama wa sehemu ya makao ya serikali  na usalama wa uwanja  wa ndege.

Mwandishi  /Mtullya Abdu/ZA /DPA.

Mhariri/Abdul-Rahman