1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

Watu watatu wauawa Iran katika kumbukumbu ya mauaji ya 2019

16 Novemba 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Norway limesema vikosi vya usalama vya Iran vimewaua kwa kuwapiga risasi waandamanaji watatu, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka mitatu ya umwagaji damu.

https://p.dw.com/p/4JaBG
Iran | Proteste in Marivan
Picha: SalamPix/abaca/picture alliance

Wanaharakati vijana wamewahimiza watu kujitoa kimasomaso na kuiteka miji ya Ahvaz, Isfahan, Mashhad na Tabriz, kati ya miji mengine ikiwa ni pamoja na mji mkuu Tehran. Maduka yalifungwa katika soko maarufu la biashara la Bazaar na viunga vyake.

Waandamanaji walimiminika barabarani baada ya kuitikia wito wa kuwakumbuka waliouawa katika ghasia za mwaka 2019, na kuongeza petroli kwenye moto kwa maandamano ya hivi karibuni yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini, binti mwenye umri wa miaka 22, aliyefariki mikononi mwa polisi wa maadili baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi ya wanawake nchini Iran.

Soma pia: 1,000 washitakiwa kwa kuandamana Iran

Kwa mujibu wa video za mtandaoni zilizothibishwa na shirika la habari la AFP, mjini Tehran, kelele za honi za magari zilisikika huku waandamanaji wakifunga moja kati ya barabara kuu kwenye uwanja wa Sanat na kupiga kelele za "Uhuru, Uhuru." Baadaye watu walimiminika kwenye mitaa ya miji mingine ikiwemo Bandar Abbas na Shiraz, ambapo wanawake walionekana wakizivua hijabu zao.

Kulingana na mtandao maarufu unaofuatilia matukio ya siasa na maandamano nchini Iran wa 1500 Tasvir, watu zaidi walijitokeza kwenye mitaa ya mji mkuu Tehran, na kuimba "Kifo kwa dikteta."

Video nyengine zilizochapishwa mtandaoni zimeonyesha purukushani kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji huku maandamano yakiendelea hadi usiku.

Shirika la Hengaw limesema vikosi vya Iran vimefyatua risasi kuzima maandamano

Iran Unruhen l Anti-Hijab-Proteste in Teheran
Polisi wakishika doria katika wilaya ya NarmakPicha: SalamPix/ABACA/picture-alliance

Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Norway, Hengaw limesema kuwa vikosi vya serikali vimefyatua risasi katika miji kulikotokea maandamano hayo kama vile Sanandaj, Kamyaran na Kermanshah. Hengaw imeliambia shirika la habari la AFP kuwa inafuatilia ripoti za mauaji mengine ya waandamanaji.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka Iran kuwaachilia mara moja maelfu ya watu waliokamatwa kwa kushiriki maandamano. Kupitia msemaji wake Jeremy Laurence, amewambia waandishi wa habari mjini Geneva, "Kufikia tarehe 12, vikosi vya usalama vimetumia nguvu kupita kiasi na kusababisha mauaji ya watu wasiopungua 326, wakiwemo watoto 43 na wanawake 25."

Soma pia: Polisi Iran yafyatua risasi, dhidi ya waombolezaji wa Amini

Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa wafanyibiashara katika soko maarufu la Bazaar waliamua kufunga maduka yao kwa kuhofia kuchomwa moto, wakati msemaji wa polisi akiiambia televisheni ya serikali kwamba watu 11 wamekamatwa kwa kosa la kuwatisha wafanyibiashara.

Kando na maandamano hayo, wafanyikazi wamegoma na wanafunzi wa vyuo vikuu wamesusia masomo yao katika wilaya ya Kurdistan, anakotokea Amini Mahsa, magharibi mwa Iran.

Maandamano hayo ya Jumanne yaliadhimisha kumbukumbu ya miaka mitatu ya kuanza kwa kile kilichoitwa "damu ya Aban"- wakati ongezeko la bei ya mafuta kulisababisha vurugu kubwa ya umwagaji damu iliyodumu kwa siku kadhaa.

Shirika la Amnesty International limesema karibu watu 304 waliuawa wakati wa maandamano hayo miaka mitatu iliyopita, japo mahakama maalum mjini London pamoja na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu yamesema ushahidi wa kitaalamu unaonyesha kuwa huenda idadi ya waliopoteza maisha yao ilikuwa kubwa zaidi na kupindukia 1,515.