Watu watano wakamatwa Chad kufuatia maandamano
17 Mei 2022Max Loalngar, msemaji wa kundi la upinzani la Wakit Tamma lililoitisha maandamano hayo, alithibitisha kuwa watu watano wamekamatwa.
Vituo saba vya mafuta ya kampuni ya Ufaransa,Total vilishambuliwa, ambapo polisi walijeruhiwa katika machafuko hayo yaliyotokea Jumamosi katika mji mkuu N'Djamena, kulingana na afisa wa polisi ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
"Viongozi watano wa maandamano" wamekamatwa, "na wanazuiliwa katika makao makuu ya idara ya usalama wa ndani," chanzo kilisema.
Nchi za Magharibi zilikubali unyakuzi
Chad imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu rais wake Idriss Deby Itno alietawala kwa miaka 30 alipouawa Aprili 2021 wakati wa operesheni za kuwaangamiza waasi kaskazini mwa nchi hiyo, na mtoto wake Mahamat Idriss Deby Itno, ambaye ni jenerali, alinyakua madaraka.
Unyakuzi huo ulikubaliwa na nchi za Magharibi, zikiongozwa na Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa nchi hiyo, ambayo inaiona Chad kama mshirika wa karibu katika mapambano yake dhidi ya wanajihadi katika Sahel.
Hivi karibuni kumekuwa na mapinduzi barani Afrika ikiwemo nchini Guinea, Mali na Burkina Faso na yamekabiliwa na vikwazo vya kikanda.
Kulingana na Loalngar, "hawahusiki na vitendo vya uharibifu. Wamekamatwa kimakosa," alisema."Polisi waliwaondoa katika eneo kuu la maandamano, kisha maandamano ya hapa na pale yakatokea baadaye sisi hatuhusiki," alisema.
Wanafunzi nao waandamana
Vyama kadhaa vya upinzani vimetoa wito wa kuachiliwa kwa waliokamatwa.
Shirika la habari la AFP lilisema mamia walishiriki maandamano hayo na bendera mbili za Ufaransa zimechomwa moto.
Siku ya Jumatatu, maandamano yaliofanywa na mamia ya wanafunzi wa shule ya upili, wengi wao wakiimba kuwa "wafaransa waondoke," yalitawanywa na polisi huko N'Djamena, AFP ilishuhudia.
Hakukuwa na mtu aliyekamatwa au kujeruhiwa, afisa wa polisi aliiambia AFP. Mwishoni mwa juma, waziri wa mawasiliano Abderamane Koullamallah alilaani ghasia hizo.
Utawala wa kijeshi ulitangaza baada ya kuchukua mamlaka kwamba utafanya "uchaguzi huru na wa kidemokrasia" ndani ya miezi 18 baada ya kuandaa kongamano la kitaifa kuhusu matatizo ya Chad.
Hata hivyo, "mazungumzo yake ya upatanisho wa kitaifa" ambayo yalikuwa yameanza Mei 10 yameahirishwa.