Watu wanaoishi kwenye ardhi iliyopoteza ubora wapo hatarini
22 Septemba 2017Kulingana na Shirika la umoja wa mataifa linalopambana na ongezeko la jangwa UNCCD, zaidi ya watu billioni moja wanaishi katika ardhi iliyopoteza ubora wake na hivyo wanakabiliwa na hatari ya janga la njaa, tatizo la uhaba wa maji na umaskini.
Matumizi ya kibinadamu ya hifadhi za asili katika kipindi cha miaka 30 iliyopita yameongezeka maradufu, na sasa theluthi moja ya ardhi ya sayari ya dunia imeharibiwa vibaya na kila mwaka miti billioni 15 na tani billioni 24 za udongo ulio na rutba hupotea, kuliingana na UNCCD.
Shirika hilo, katika ripoti yake, linasema ardhi tunayoishi inaelemewa na kwamba urejeshaji na uhofadhi ni mambo muhimu ili kuweza kuinusuru. Shirika hilo la UNCCD linafanya kampeni ya kulinda ardhi na ndiyo mkataba pekee wa kimataifa unaofunganisha kisheria kuhusu masuala ya ardhi.
Naibu katibu mtendaji wa UNCCD Pradeep Monga anasema kadiri ardhi inapopunguza uzalishaji, jambo ambalo linaweza kusababishwa na ukataji miti, malisho ya wanyama kupita kiasi, mafuriko na ukame, watu hulaazimika kuhamia mijini au ughaibuni, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea migogoro juu ya rasilimali zinazopungua, na uchumi wa mataifa unaathirika pakubwa.
Na ikiwa kiasi cha ardhi ya uzalishaji kinapungua, hakutakuwepo na ya kutosha kulisha idadi kubwa ya watu duniani, inayokadiriwa kuongezeka kwa hadi ya watu billioni 9 kufikia mwaka wa 2050 kutoka billioni saba ya sasa.
Monga anasema ikiwa tunaweza kuzuwia uharibifu wa ardhi na kuzuwia jangwa kwa kupanda miti, tunaweza kupata usalama wa chakula. Anasema mambo madogo kama vile familia kupunguza utupaji wa chakula, na kuboresha usimamizi wa ardhi, njia za kisasa za kilimo, na sera za kitaifa zinazonuwia uharibifu wa ardhi yanaweza kuleta tofauti kubwa.
Monga anasema China, ambayo ndiyo nchi ilioanzisha sheria ya kwanza duniani kuzuia na kudhibiti kuenea kwa jangwa mwaka wa 2002, imefanikiwa kuotesha miti katika maelfu ya hektea ya jangwa la Mongolia, na hivyo kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula, ajira zaidi na maisha bora kwa wakaazi wa eneo hilo.
Uharibifu wa ardhi unaweza ukadhibitiwa iwapo mataifa yatawekeza katika mipango mizuri ya kukabiliana na ukame itayoweza kuwaokoa wengi na majanga na kuboresha mazingira, anasema naibu katibu mtendaji wa UNCCD Pradeep Monga.
Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga