1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu tisa wauawa kwa kukanyagwa na lori Berlin

19 Desemba 2016

Lori limeugonga umati mkubwa wa watu na kuwakanyaga watu kadhaa katika barabara moja mjini Berlin na kusababisha vifo vya watu tisa na wengine 50 kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/2UZJB
Deutschland Polizei geht von Anschlag auf Berliner Weihnachtsmarkt aus
Picha: Reuters/F. Bensch

Vibanda kadhaa vya masoko ya Krismasi vilivyoharibiwa vimeonekana karibu na kanisa la Kaiser-Wilhelhm magharibi ya Berlin, kwa mujibu wa video ya gazeti la Berliner Morgenpost katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook. Magari kadhaa ya polisi yameonekana katika eneo la tukio. Polisi wameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kuwa wanalichukulia tukio hilo kuwa la kigaidi.

Vyombo vya habari, vikiwanukuu polisi katika eneo hilo, vimesema dalili za awali zinaashiria shambuio dhidi ya soko hilo linalopatikana karibu na barabara ya nguo za mitindo ya Kurfuerstendamm na karibu na kanisa la makumbusho la Kaiser Wilhelm lililowekwa kama magofu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Mshukiwa atiwa mbaroni

Msemaji wa polisi amesema dereva wa lori hilo amekamatwa karibu na eneo la tukio. Msaidizi wa dereva huyo amekufa katika tukio hilo ambalo polisi wanasema huenda ni shambulizi la kigaidi. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefahamishwa kuhusu balaa hilo na waziri wa mambo ya ndani, Thomas de Maiziere na meya wa mji wa Berlin, Michael Müller.

Deutschland Möglicher Anschlag auf Berliner Weihnachtsmarkt
Picha: REUTERS/P. Kopczynski

Tukio hilo limeibua kumbukumbu za shambulizi lililotokea nchini Ufaransa mnamo mwezi Julai mwaka huu wakati raia wa Tunisia Mohamed Lahouaiej Bouhlel alipeleka lori la tani 19 karibu na fukwe ya bahari mjini Nice, na kuwagonga watu waliokuwa wamekusanyika kutazama mafashifashi wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru, na kuwaua watu 86. Polisi walimpiga risasi dereva huyo aliyefanya shambulizi hilo lililodaiwa kufanywa na kundi linalojiita dola la kiislamu.

Picha za televisheni kutoka Berlin zimeonyesha lori likiwa limesimama katika takataka za vibanda vya mbao vinavyojumuisha soko la Krismasi la "Christkindlmarkt". Masoko haya yanapatikana katika maeneo kadhaa ya Berlin msimu huu wa mwaka.

Mwandishi:Josephat Charo/dpa/afpe/reuters

Mhariri:Mohammed Khelef