1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu sita wakisiwa kufa katika tukio la Daraja la Baltimore

27 Machi 2024

Wafanyakazi wote sita waliotoweka baada ya Daraja la Francis Scott Key mjini Baltimore, kuporomoka jana Jumanne wanakisiwa kuwa wamefariki. Shughuli ya kuwatafuta imesitishwa hadi Jumatano asubuhi.

https://p.dw.com/p/4e9np
Meli ya mizigo ililigonga Daraja la Francis Scott Key
Daraja la Francis Scott Key liliporomoka na kutumbukia majini baada ya kugongwa na meli ya shehena za makontenaPicha: Tasos Katopodis/Getty Images

Mkuu wa polisi wa jimbo la Maryland Roland L. Butler Jr., amesema Jumanne jioni kuwa operesheni ya utafutaji na uokozi sasa inabadilishwa kuwa ya utafutaji wa miili.

Soma pia: Watu wawili wauawa, wengine kadhaa wajeruhiwa katika shambulizi la bunduki Baltimore

Amesema wapiga mbizi watarejea katika eneo la mkasa hii leo saa kumi na mbili asubuhi, wakati mazingira magumu ya usiku yanatarajiwa kuimarika.

Meli kubwa ya shehena iligonga nguzo ya daraja hilo na kusababisha kuvunjika katika vipande na kutumbukia majini. Gavana wa Maryland alisema wahudumu wa meli hiyo walituma ujumbe wa dharura wa kuomba msaada muda mfupi kabla ya tukio hilo kutokea, hatua iliyowasaidia maafisa kupunguza idadi ya magari kwenye daraja hilo.