Watu saba wauwawa nchini Somalia
26 Machi 2008Wapiganaji wa kiislamu nchini Somalia wameuteka mji wa Jowhar kusini mwa nchi hiyo hii leo katika uvamizi uliosababisha vifo vya watu wasiopungua saba. Wakati huo huo, mashirika ya misaada ya kimataifa yanasema Somalia ni nchi hatari kwa wafanyakazi wake kuwahudumia waathirika wa vita.
Wakaazi na maafisa wa mji wa Jowhar wanasema wanamgambo wa kiislamu zaidi ya 100 waliokuwa wamejihami na silaha nzito wameuteka na kuudhibiti kwa muda mji huo wenye shughuli nyingi za kilimo. Uvamizi huo wa kushangaza umesababisha watu saba kuuwawa, akiwemo mtoto mmoja.
Wapiganaji wa kiislamu waliovurumisha magrenedi yanayosukumwa na maroketi na kufyatua risasi, wamewashinda nguvu wanajeshi wa serikali ya Somalia na kuwakomboa wafungwa katika uvamizi huo wa alfajiri mjini Jowhar, yapata kilomita 90 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu. Washambuliaji wote wameondoka mjini humo leo asubuhi.
Mkaazi wa mji wa Jowhar, Aden Yusuf, anasema ameziona maiti tano za wanajeshi wa Somalia na maiti mbili za raia zikiwa zimezagaa katika barabara za mji huo.
Mkaazi mwingine wa mji huo, Abdi Ali Osman, ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba watu saba, akiwemo mwanamke mmoja aliyekuwa mwanajeshi wa serikali pamoja na mtoto wake aliyekuwa amembeba mgongoni, wameuwawa na wapiganaji wa mahakama za kiislamu.
Ameongeza kusema kuwa wapiganaji hao baadaye waliwakomboa wafungwa katika mji wa Jowhar, ambao ulikuwa ukidhibitiwa na meya wa mji wa Mogadishu, mbabe wa zamani wa kivita, Mohamed Dheere.
Mji wa Jowhar ni mji muhimu zaidi kati ya miji iliyowahi kushambuliwa na wanamgambo wa kiislamu wa Somalia katika miezi michache iliyopita na uvamizi wa leo unadhihirisha kushindwa kwa serikali ya mjini Mogadishu kuweza kuonyesha madaraka yake, licha ya kuungwa mkono na majeshi ya Ethiopia na vikosi vya Umoja wa Afrika.
Wapiganaji wa mahakama za kiislamu walikuwa wameiteka miji minne midogo pamoja na kituo cha upekuzi cha kijeshi karibu na mji mkuu Mogadishu kabla uvamizi wa leo katika mji wa Jowhar.
Wanamgambo wa al Shabaab
Wakati huo huo, viongozi wa mji wa bandari wa Merca, kilomita 100 kusini mwa Mogadishu, wamesema wanajeshi wa Ethiopia wamekuwa wakiudhibiti mji huo tangu Jumapili iliyopita.
Mmoja wa viongozi hao, Mohamud Kulow Aweys, amesema wanajeshi wa Ethiopia waliwaita viongozi wa mji wa Merca na kuwambia wameingia mjini humo kutokana na kuwepo kwa hali mbaya ya usalama na kwamba makundi ya al Shabaab yamo mjini humo.
Marekani imeliorodhesha kundi la al Shabaab la Somalia kuwa la kigaidi ili kuongeza shinikizo la kile Marekani inachokiita kuwa kiungo muhimu cha kundi la al Qaeda nchini Somalia.
Ripoti ya mashirika ya misaada
Hii leo mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada yametoa taarifa inayosema kuwa Somalia ni nchi hatari kwa wafanyakazi wake kuweza kuwasaidia zaidi ya Wasomali milioni moja wanaoishi katika hali ngumu kutokana na athari za vita.
Mashrikia 39 yakiwemo Oxfam, World Vision na Save the Children, yameonya juu ya janga kubwa la kibinadamu linalokaribia kutokea nchini Somalia huku baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likijiandaa kuijadili hali nchi humo katika kikao chake kitakachofanyika hapo kesho mjini New York nchini Marekani.
Bi Verity Johnson, wakili mkuu wa shirika la Oxfam mjini Nairobi, amesema wameitoa ripoti hiyo kutokana na hali mbaya. ´Tumeitoa taarifa hii wakati huu kwa sababu ya hali kuendelea kuzorota nchini Somalia. Tulionya miezi mitano iliyopita kuhusu jambo hili na sasa tunachosema ni kwamba hali imezidi kuwa mbaya.´
Baraza la usalama limedurusu uwezekano wa Umoja wa Mataifa kujihusisha zaidi nchini Somalia, lakini nchi wanachama zimepinga kupeleka kikosi kamili cha kulinda amani nchini humo.
Umoja wa Mataifa unatafakari kuwahamishia wafanyakazi wake wanaoshughulikia maswala ya Somalia walio mjini Nairobi Kenya, hadi mjini Mogadishu ili kuongeza uwepo wake nchini Somalia. Kuna chaguo lengine pia la kupeleka kikosi cha wanajeshi na polisi 28,500 wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia au kutuma kikosi cha wanajeshi 8,000 kuiimarisha hali nchini humo.
Mashirika ya misaada katika ripoti yao yanasema mateso yanayowakabiliwa wasomali ambayo yamewalazimu kuyakimbia makazi yao, yamezidi kufanywa kuwa magumu na mambo mengine. Bei za juu za vyakula, mfumuko mkubwa wa bei na ukame katika maeneo mengi nchini inaziweka jamii katika hali ya kutapatapa ili kuendelea kuishi.
Ripoti inasema jamii zilizouhama mji wa Mogadishu au wale walio maskini hohehahe ambao hawakuwa na uwezo wa kukimbia, walipokea mshahara wa takriban dola 12.13 kila mwezi. Huduma za utoaji misaada zimefujwa na ukosefu wa utawala wa sheria na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama.
Bi Verity amesema, ´Watu elfu 360 wamelazimika kuyahama makazi yao na nusu milioni wanahitaji msaada ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miezi michache iliyopita. Bado tunakabiliwa na changamoto zile zile tukijaribu kuwafikia watu hao.´
Mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa misaada, wizi wa vyakula vya misaada na kutoheshimiwa kwa sheria za kimataifa na pande zote husika, kumesababisha Wasomali milioni mbili kuhitaji msaada msingi wa kibinadamu.
Wafanyakazi sita wa misaada wameuwawa nchini Somalia tangu mwanzoni mwa mwaka huu hivyo kuyalazimu mashirika ya misaada kuwaondoa wafanyakazi wao. Visa vya utekaji nyara pia vimeongezeka.
Verity Johnson amelitolea mwito baraza la usalama liushughulikie mgogoro wa Somalia.
´Kwa hiyo tunalitolea mwito baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liushughulikie mzozo wa Somalia ili mashirika ya misaada yaweze kufanya kazi ya kuwasaidia watu wanaoteseka.´
Vituo vya upekuzi visivyo halali na vizuizi vya barabarani vimeongezeka kutoka 147 mwezi Januari mwaka jana hadi kufikia 396.
Ripoti ya mashirika ya misaada imesema juhudi za kuwasaidia Wasomali hazijatatizwa kufikia kiwango cha hivi sasa. Imezungumzia sheria za kuchelewesha usafirishaji wa bidhaa, kushambuliwa kwa wafanyakaziw a misaada, makundi ya kijamii na vyombo vya habari, na serikali kushindwa kushughulikia visa vya ukiukaji wa usalama inavyoweza kuvishughulikia.