1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 50 wapotezewa makaazi duniani

20 Juni 2014

Zaidi ya watu milioni 50 walilazimishwa kuhama makazi yao duniani kote kufikia mwishoni mwa mwaka jana, hicho kikiwa ni kiwango kikubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

https://p.dw.com/p/1CMnS
Wakimzi wa Somalia katika kambi ya Dadaab Kenya.
Wakimzi wa Somalia katika kambi ya Dadaab Kenya.Picha: Oli Scarff/Getty Images

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Ijumaa (20.06.2014) inayalaumu mataifa makubwa duniani kwa kutochukuwa hatua ya kukabiliana na ongezeko hilo kubwa sana la ghafla la wakimbizi duniani ambapo watu wamekuwa wakiikimbia mizozo kuanzia Syria hadi Sudan Kusini.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba nusu ya wakimbizi hao ni watoto, wengi wao wakiwa wamenaswa kwenye mizozo au ukandamizaji ambao mataifa makubwa yenye nguvu duniani yameshindwa kuizuwiya au kuikomesha.

Idadi ya jumla ya watu milioni 51.2 waliopotezewa makaazi yao duniani imeongezeka kwa watu milioni sita kwa kulinganisha na mwaka 2012. Idadi hiyo ni pamoja na wakimbizi milioni 16.7 na watu milioni 33 waliopotezewa makaazi yao ndani ya nchi zao na watu milioni 1.2 wanaotafuta hifadhi ambao maombi yao bado yamekwama.

Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres akizungumza na waandishi wa habari juu ya ongezeko hilo kubwa la wakimbizi wakati akizinduwa ripoti yao hiyo mjini Geneva amesema.

"Sio tu tunakabiliwa na hali ya kuongezeka kwa wakimbizi,kwa kweli tunakabiliwa na ongozeko kubwa sana la ghafla, ongezeko kubwa mno la watu wanaolazimika kuhama makaazi yao duniani."

Wakimbizi wa Syria ndio wengi

Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Wasyria wanaoukimbia mzozo wa nchi yao unaozidi kupamba moto wamefikia milioni 2.5 miongoni mwa wakimbizi wapya duniani mwaka jana.

Wakimbizi wa Syria karibu na mpaka wa Uturuki.
Wakimbizi wa Syria karibu na mpaka wa Uturuki.Picha: Reuters

Kwa jumla karibu wakimbizi milioni tatu wa Syria wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani za Lebanon, Uturuki,Iraq na Jordan wakati wengine milioni 6.5 wamepotezewa makaazi yao ndani ya Syria kwenyewe.

Mizozo iliozuka mwaka huu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,Ukraine na Iraq inazifanya familia zaidi kukimbia makaazi yao na kuzusha hofu ya kuwepo kwa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Iraq.

Chanzo cha ongezeko

Guterres amesema wanashuhudia gharama kubwa zinazotokana na kushindwa kukomesha vita, kushindwa kutatua au kuzuwiya mizozo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukuwa hatua katika kukabiliana na mizozo mingi mikubwa duniani.

Guterres amesema ongezeko hilo linatokana na ukweli kwamba wanaishi katika dunia ambapo mizozo inazidi kuongezeka katika njia isiotabirika wakati huo huo ya zamani inaonekana kutomalizika.

Antonio Guterres Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa akiwasilisha repoti yao Geneva.(19.06.2014)
Antonio Guterres Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa akiwasilisha repoti yao Geneva.(19.06.2014)Picha: DW/Claudia Witte

Ameongeza kusema jumuiya ya kimataifa haina uwezo mkubwa wa kuzuwiya mizozo na kuitatuwa kwa wakati muafaka.

Raia wa Afghanistan,Syria na Somali hufanya kama asilimia 53 ya wakimbizi milioni 11.7 walioko chini ya dhamana ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. Wapalestina milioni tano wako chini ya uangalizi wa shirika ndugu la UNRWA.

Asilimia 86 ya wakimbizi duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea kinyume na inavyofikiriwa kwamba wamefurika kwenye nchi zilizoendelea.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef