1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 50 kuhamishwa kwa mafuriko duniani

4 Desemba 2019

Wakati macho ya ulimwengu yakielekezwa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP25), inaelezwa kwamba zaidi watu milioni 50 watalazimika kuyakimbia makaazi yao kila mwaka kufikia mwishoni mwa karne hii.

https://p.dw.com/p/3UBzu
Südsudan Überschwemmungen Hütten
Picha: Getty Images/AFP/P. Louis

Matokeo ya utafiti yaliyochapishwa siku ya Jumanne (Disemba 3) mjini Madrid na Taasisi Inayochunguza Ukimbizi wa Ndani cha Geneva (IDMCS) inasema kuwa kiwango hicho kitakuwa ni mara tano zaidi ya hali ilivyokuwa baina ya mwaka 1970 na 2005, ambapo watu milioni 10 walilazimika kuhama makaazi yao kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. 

Kuongezeka kwa idadi hiyo kunachangiwa na ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni wakati pia viwango vya mvua vikiongezeka na mapande ya barafu yakiyeyuka kutokana na joto kuwa kali kwenye sayari ya dunia. 

"Matokeo ya hayo ni mafuriko makubwa na ya mara kwa mara", alisema mwandishi wa utafiti huo, Justin Ginnetti, akifafanuwa kuwa "nusu ya ongezeko la wakimbizi wa ndani litachochewa na athari za mabadiliko ya tabia nchi na nusu yake itatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu."

Idadi ya watu watakaolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na mafuriko ya mito itafikia hadi milioni 20 kwa mwaka, endapo serikali hazitaongeza jitihada za kudhibiti kiwango cha joto ulimwenguni kuwa chini ya nyuzi 1.5, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Watu milioni 20 waligeuka wakimbizi 

Viongozi wa dunia wanaoshiriki mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi mjini Madrid, COP25.
Viongozi wa dunia wanaoshiriki mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi mjini Madrid, COP25.Picha: picture-alliance/dpa/M. Fernandez

Siku ya Jumatatu Disemba 2), shirika la misaada la Uingereza, Oxfam, lilisema kuwa hali ya mbaya ya hewa na moto kwenye misitu mikubwa viliwafanya zaidi ya watu milioni 20 kukimbia makaazi yao ndani ya muongo mmoja uliopita, na tatizo hili huenda likawa kubwa zaidi. 

Hata hivyo, ripoti hiyo ya IDMC inasema kuwa kuna baadhi ya mifano mizuri ya juhudi za kuwakinga watu wasilazimike kuhama kutokana na mafuriko, zikiwemo za mipango miji ambayo hairuhusu watu kujenga nyumba katika maeneo hatari na uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya uokozi kwa wale wanaokabiliwa na mafuriko.

Baadhi ya nchi za Asia, hasa India, Bangladesh na China, zimefanikiwa kuwahamisha mamilioni ya watu siku kadhaa kabla ya vimbunga, na kwa mujibu wa mwandishi wa ripoti hiyo, Justin Ginnetti, juhudi hizi zinapaswa kuigizwa kwengineko duniani, hasa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara.

Wapanga mikakati kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi waliunda chombo mwaka 2013 cha kushughulikia madhara na hasara zinazosababishwa na mabadiliko hayo, ikiwemo watu wanaolazimika kuyakimbia makaazi yao, lakini wanaharakati wa mazingira wanasema utekelezaji wa hatua hizo umekuwa ukienda taratibu.