Watu mashuhuri na miaka 50 ya DW
16 Januari 2013"Ningependa kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Deutsche Welle kwa kazi nzuri munayoifanya ya kukikuza Kiswahili kwamba ni katika miongoni mwa redio za mwanzo kutumia Kiswahili. Katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Afrika ya Kat, Deutsche Welle imekuwa na umaarufu mkubwa sana. Kupitia kwenu, hata wale ambao Kiswahili si lugha yao ya kwanza wameweza kujifunza mengi. Pia mumekuwa wawazi kutangaza matukio mbali mbali yanayotokea hasa pale unapotokea ukandamiazaji wa haki za wananchi, penye dalili ya uimla au udikteta mumekuwa hamutafuni maneno.“ - Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar.
“Kituo chetu kinafanya kazi vizuri na Deutsche Welle hasa Idhaa ya Kiswahili kwa sababu Watanzania wengi tunaongea Kiswahili kwa hiyo watu wanasikiliza Kiswahili. DW inatoa taarifa ambazo zinasambaa nchi nzima. Tumekuwa tukipokea taarifa na watu wamekuwa wakituambia taarifa hii nimeisikia DW wengine wamekuwa wakituambia kwa kusikiliza DW tumekuwa tukiwasikia ninyi na kusikia taarifa mbali mbali, kwahiyo DW imekuwa ni nzuri sana au ni sauti ambayo sisi ambao tunazungumza mambo ya kuwafikia watu na watu kuweza kuzungumza masuala yao kupitia redio hii.” - Helen Kijo Bisimba, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania.
“Mimi nimeanza kuisikiliza Deutsche Welle kwa muda mrefu sana, miaka ya ‘60 nikiwa mwanafunzi wa shule za msingi nilikuwa namsikia baba anafungua DW wakati nikiwa sekondari hata nikiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam nilikua napenda sana kusikiliza redio yenu. Uzuri wa taarifa ya habari na matangazo mengine yanayotoka kwenye DW ni kwamba ni ya uhakika ambayo mtu akiyasikiliza hawi na wasi wasi. Kwa hiyo ni redio yenye heshima na sifa kubwa sana nchini mwetu na pembe nyengine za Afrika.” - Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini Tanzania
"DW imekuwa ni chombo kinachounganisha sauti zetu. Unajua vyombo vya habari vinasaidia kueleza kuwafahamu watu wa nchi mbali mbali kwa hiyo mumekuwa mukiunga bara la Afrika na sehemu nyingine duniani. Tumepata fursa ya kufahamu mambo yanayotokea sehemu mbali mbali. Ya pili ni Kiswahili. Nataka niwapongeze kwa hilo kuweka lugha ya Kiswahili na kuitumia kwa kuwaelewesha wazungumzaji wa Kiswahili. Mimi nadhani hiyo ni kati ya vitu ningependa kuwapongeza.“ - Getrude Mongella, Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika.
“Naipongeza DW kwa kutimiza miaka 50.ANaona ni nafasi adhimu kwa Idhaa ya Kimaifa kutangaza kwa lugha nyingi za kando. Kwa sababu kama mimi najifunza pia tamaduni za lugha nyengine. Hivyo ni muhimu kuona kuwa hata tamaduni za jamii tofauti zinazingatiwa, mawasiliano yanafika hadi kwenye ngazi za chini na matumaini ya wasikilizaji yanatimizwa na hivyo DW inafanya kazi kubwa kwa ajili yetu.“ - Auma Obama, Dada wa Rais Barack Obama wa Marekani.
“Hongereni sana maana munatusaidia sana kueneza sifa ya Kiswahili duniani na Kiswahili ni lugha moja ambayo inakuwa zaidi ya lugha nyingi duniani. Hivi karibuni kwa kweli Kiswahili kitakuwa lugha moja ya dunia ikishindana na lugha nyengine, kama vile Kiingereza, Kitaliana au Kihispania.“ - Prof. Ngugi wa Thiong'o, Mwandishi na Mhadhiri wa Fasihi kutoka Kenya.
“Deutsche Welle ni redio ambayo mimi mwenyewe nimekuwa naisikiliza tangu nikiwa mdogo sana, tangu nikiwa shule ya sekondari,sio tu kwa sababu ya unadhifu wa lugha inayotumika yaani Kiswahili. DW imetoa mfano kwamba katikati ya bara la Ulaya kuna redio inazungumza Kiswahili na kusikika katika maeneo mengi sana. Sasa hivi sio nchi za Afrika ya Mashariki lakini hata Afrika ya Kati. Mimi mwenyewe nimekuwa Rwanda nimekuwa Congo nimeweza kusikiliza DW. Muendelee na tunawatakia kila la heri na muongeze vipindi ambavyo vitarutubisha lugha yetu ya kiswahili na wasikilizaji waongezeke zaidi na zaidi.“ - Balozi Augustine Mahiga, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Tanbihi: Hizi ni kauli za watu mbalimbali mashuhuri barani Afrika kuhusiana na Idhaa ya Kiswahili ya DW na maadhimisho yake ya miaka 50. Picha kubwa ya juu imechorwa na Frank Yustard Ngimbwa wa Dar es Salaam, Tanzania.
Mhariri: Mohammed Khelef