Watu kumi wauawa na waasi mashariki mwa DRC
21 Mei 2018Afisa wa serikali ya jimbo Donat Kibwana, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa waasi wanaoaminika kutoka kundi la ADF walishambulia kijiji cha Manggboko katika mkoa wa Beni Jumapili usiku, na kuuwa watu 10 wakiwemo wasichana wawili.
Mwandishi wa DW katika mkoa wa Beni John Janyunyu ametembelea familia moja iliyopmpoteza baba mzazi ambapo ameelezea huzunu kutawala katika familia hiyo.
"Na unapoingia Mbau, utaona nyuso za watu zikiwa zimekunjana kufuatia mauaji hayo ya jana jioni katika kata ya Mangboko," ameripoti Kanyunyu.
Jeshi lakwepa wajibu wake
Philippe Paluku Bonane, kiongozi wa kiraia, aliiambia dpa kuwa jeshi halikuingilia kati mauaji hayo hadi waasi walipoondoka kijijini hapo. Mashirika ya kiraia katika wilaya ya Beni, yametangaza siku mbili za maombolezo kuanzia Jumatatu.
Aidha mashirika ya kiraia yametoa mwito kwa serikali kufanya juu chini ili kuhakikisha kuwa mauaji na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF kutoka Uganda yanakomeshwa.
Makundi mbalimbali ya waasi yanaendesha shughuli zake mashariki mwa Congo, yakipigania hasa udhibiti wa rasilimali za eneo hilo.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, kundi la ADF liliundwa mwaka 1995 na wanakutikana kwenye eneo la milima mpakani mwa DRC na Uganda. Kundi hilo linafahamika kwa kutumia wanajeshi watoto.
Kundi hilo limeuawa takribani watu 2000 katika mji na Wilaya ya Beni katika kipindi cha miaka minne, ameripoti mwandishi wa DW John Kanyunyu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef