Watu kadhaa wauliwa katika shambulio la bomu harusini
18 Agosti 2019Zaidi ya watu 1,000 walialikwa, amesema mtu mmoja aliyeshuhudia, wakati hofu ikitanda kuwa inaweza kuwa shambulio baya kabisa kuwahi kutokea mjini Kabul mwaka huu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Nusrat Rahimi ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mshambuliaji alijiripua miongoni mwa washiriki wa sherehe hiyo ya harusi. Kundi la Taliban na washirika wake wa ndani wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu hufanya mashambulizi ya umwagaji damu katika mji mkuu huo.
Mripuko huo ulitokea karibu na jukwaa ambako wanamuziki walikuwa na "vijana wote , watoto na watu wote ambao walikuwa katika eneo hilo waliuwawa," mtu aliyeshuhudia Gul Mohammad alisema. Mmoja kati ya waliojeruhiwa , Mohammad Toofan, alisema kwamba "wageni wengi waliuwawa."
Maafisa hawakutarajiwa kutoa idadi yoyote ya waliofariki hadi leo Jumapili (18.08.2019).
Miili ya watu imetapakaa ukumbini
"Kuna watu wengi waliofariki na kujeruhiwa," alisema Ahmad Omid, aliyenusurika ambaye alisema kiasi wageni 1,200 walialikwa katika harusi hiyo ya mpwa wa baba yake. "Nilikuwa na bwana harusi katika chumba kingine ambako tulisikia mripuko huo na kisha sikuweza kumpata mtu yeyote. Kila mtu alikuwa amelala chini katika ukumbi huo."
Nje ya hospitali mjini humo, wana familia walikuwa wakilia. Wengine walitapakaa damu.
Mripuko huo katika ukumbi wa harusi wa dubai City magharibi mwa Kabul, sehemu ya mji huo ambayo wanaishi, wengi ni watu wa kabila la wachache wa jamii ya washiia wa Hazara, walifikisha mwisho kipindi cha utulivu.
Agosti 7 , shambulio la bomu lililokuwa katika gari lililofanywa na kundi la Taliban lililolenga vikosi vya majeshi ya usalama ya Afghanistan liliripuka katika barabara hiyo hiyo, na kuwauwa watu 14 na wengine 145 walijeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na raia wengine.
Kumbi kubwa za harusi mjini Kabul zilizopambwa vizuri na kuwa na taa nyingi ni vituo vya maisha ya jamii katika mji huo unaoandamwa na vita kwa miongo kadhaa, ambapo maelfu ya dola hutumika katika usiku mmoja.
"Tumefadhaishwa na taarifa za shambulio la kujitoa muhanga katika ukumbi wa harusi mjini Kabul. Uhalifu wa kiwoga dhidi ya watu wetu; inawezekana vipi kumfunza binadamu na kumwambia aende kujiripua ndani ya harusi ? !! Sediq Seddiqi, msemaji wa rais Ashraf Ghani, amesema katika maandishi katika ukurasa wa Twitter.