1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katika masaa 24, makabiliano yalikuwa makali zaidi

Faiz Musa12 Aprili 2019

Kiasi cha watu 75 wameuawa katika kipindi cha wiki moja cha makabiliano yanayoendelea nchini Libya baina ya kikosi cha mbabe wa kivita, Khalifa Haftar, na jeshi la serikali inayoungwa mkono kimataifa mjini Tripoli.

https://p.dw.com/p/3GfaX
Libyen Zusammenstößen zwischen Haftars Streitkräften und den GNA-Streitkräften
Picha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Mwakilishi wa WHO nchini Libya, Daktari Syed Jaffar Hussain, alisema kwamba miongoni mwa hao, raia saba wameuwawa na kumi kujeruhiwa na wanahofia kuzuka kwa maradhi ya kuambukiza kutokana na maji machafu na watu kukimbia sehemu za vita karibu na mji wa Tripoli.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephan Dujarric, alisema katika kipindi cha masaa 24, makabiliano yalikuwa makali zaidi tangu kuanza kwa vita hivyo katika maeneo yanayozunguka mji wa Tripoli na zaidi ya raia elfu tisa na mia tano wameyakimbia makaazi yao.

"Wenzetu wa huduma za kijamii wameripoti kwamba bado watu wanaendelea kuyahama makaazi yao katika maeneo yanayoathirika na vita yanayozunguka mji wa Tripoli. Kiasi cha familia 650 zimeomba kuhamishiwa maeneo salama. Ila kwa sababu ya ugumu wa kuwafikia, vita na matumizi ya ovyo wa silaha, vikundi vya uokozi vimeweza kuwasaidia asilimia 15 pekee. Operesheni nyengine za uokoaji zinaendelea hii leo. Familia zilizokwama katika sehemu zilizo na vita hazihofii tu usalama wao bali pia kuishiwa na huduma za kimatibabu," alisema Dujarric.

Libyen Kämpfe um Tripolis
Vikosi kutoka jeshi la Mashariki wamekaa chini baada ya kukamatwa na jeshi la TripoliPicha: Reuters/I. Zitouny

WHO iliwasilisha vifaa vya matibabu na dawa kwa hospitali mbali mbali ila ilisema kuwa dawa hizo zitatosheleza kwa muda wa wiki mbili tu, hata hivyo wameweka mipango iwapo mamia ama maelfu ya raia wengine watawachwa bila ya makaazi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la utaratibu wa misaada ya kiutu, OCHA, liliripoti kwamba kiasi cha watu elfu tatu na mia tano wameyakimbia makaazi yao mjini Tripoli katika kipindi cha masaa 24 na asilimia tisiini ya walioomba kuhamishwa hawakuwezekana kupelekwa mahala salama.

Libyen Kämpfe um Tripolis
Wanajeshi wa Tripoli wakiwa katika kizuizi cha Ain Zara kusini mwa TripoliPicha: Reuters/I. Zitouny

Waziri wa Ulinzi wa Tunisia Abdelkarim Zbidi alisema nchi yake imeliweka katika hali ya tahadhari jeshi la wanamaji, angani na ardhini katika sehemu wanazopakana na Libya.

Vita hivyo vimetishia usafirishaji wa mafuta, kuongeza idadi ya wahamiaji katika bahari ya Mediterrania kuelekea Ulaya na vile vile kurudisha nyuma mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa na kuyapa nguvu makundi ya waliyo na silaha.

(RTRE/APE/AFPE)