Watu 8 wauwawa katika shambulizi Burundi
10 Mei 2021Shambulizi hilo limetokea karibu na mkoa wa Muramvya katikati mwa Burundi, ambako kabla ya kutokea shambulio hilo Rais Evariste Ndayishimiye alikuwa katika mkoani huo akihudhuria ibada ya Misa. Mmoja wa walouwawa katika shambulio hilo ni afisa wa jeshi anaye hudumu katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kusimamia amani nchini
Somalia.
Tamko la wizara ya mambo ya ndani na maendeleo ya jamii na usalama limesema watu wa 8 wameuwawa na wengine kadha kujeruhiwa katika shambulizi lililoendeshwa na wahalifu wenye silaha, dhidi ya magari ma-4 ya uchukuzi, si mbali na mkoa wa Muramvya katikati mwa nchi.
Waliofanya shambulizi wahalifu waliokuwa wamejihami kwa silaha
Miongoni mwa walio poteza maisha katika shambulio hilo ni pamoja na Kanal Michel Nizigiyimana, afisa wa jeshi la Burundi anaye hudumu katika kikosi cha Umoja wa mataifa cha kusimamia amani Somalia AMISOM ambaye ameuwawa pamoja na mwanaye huku mkewe akitajwa kujeruhiwa
vikali.
Wizara ya mambo ya ndani na usalama imewataja waloendesha shambulio hilo kuwa ni wahalifu wenye silaha. Duru kutoka maeneo ya tukio zinasema waliopoteza maisha katika shambulio hilo wamefikia idadi ya watu 12 na kwamba baadhi ya majeruhi tayari wamepekekwa katika hospitali za mji mkuu Bujumbura.
Pia duru hizo zinasema walohusika na shambulio hilo walipora vitu vya abiria katika magari hayo.
Shambulio hilo limetokea masaa kadhaa baada ya rais Evariste Ndayishimiye kuutembelea mkoa huo wa Muramvya Jumapili iliyopita alikohudhuria ibada ya misa na kusema katika hutuba yake kanisani kuwa
hapendelei kuiongoza nchi yenye watu wasio na upendo.
Burundi iko katika kipindi kigumu
Sipendelei kuwaongoza watu wasio na upendo, wasopendana na wala sipendelei kuwaongoza watu wasio na afya nzuri. Napendelea kuona nchi hii ikiwa nchi ya watu wenye utu, vigezo hivyo Mungu alitupatia kilicho salia ni sisi kuvitumia.
Rais Ndayishimiye amebaini kuwa nchi iko katika wakati mgumu kwani ilipitia maovu mengi na makubwa. Na kwamba huu ni wakati wa kurejesha utangamano.
Tayari rais Evariste Ndayishimiye ametowa risala rasmi kupitia mtandao wake wa Twitter na kusema kusikitishwa na mauwaji hao. Na pia ametowa salamu za rambi rambia kwa familia zilopoteza watu wao katika shambulizi hilo na kwa nchi zima.
Shambulizi hilo ni la kwanza la aina hiyo kutokea nchini humu tangu Rais Evariste Ndayishimiye kushika hatamu za uongozi wa Burundi mwezi Juni mwaka 2020.