Watu 60 wameuawakwa ajali Kusini mwa Ghana.
22 Machi 2019Kamamda wa polisi Antwi Gyawu ameliambia shirika la habari la AFP kwamba magari hayo yalikuwa yakitokea pande tofauti wakati ajali hiyo ilipotokea. Kamanda Gyawu amesema katika ajali hiyo iliyoua wato 60 moja ya mabasi hayo lilishika moto huku jingine likiharibiwa vibaya.
Mabasi hayo yanakadiriwa kuwa yalikuwa yamebeba 50 kila moja. Watoa huduma za dharura waliwasili katika eneo la tukio ikiwa ni pamoja na vikosi vya kuzima moto ili kuzima moto uliolipuka kutokana na ajali hiyo. Daktari Kwame Arhin katika wa Hospitali ya serikali ya Kitampo amesema watu 28 wamefikishwa hospitalini hapo kutokana na majeraha.
Dk. Arhin ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu 7 kati ya 28 waliofikishwa hospitalini hapo wako kwenye hali mbaya na wengi wamepata majeraha makubwa vichwani, na pia miili ya watu kadhaa waliofariki kwenye ajali hiyo imehifadhiwa Hospitalini hapo.
Uchunguzi wa ajali waendelea
Ingawa chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa mmoja wa madereva wa mabasi hayo alishindwa kulidhibiti basi kutokana na kuzidiwa na usingizi. Kamanda wa kikosi cha zimamoto wa eneo la Kitampo kulikotokea ajali hiyo Ankomah Twene, amesema abiria walionusurika wamewaambia kuwa dereva wao alikuwa akisinzia lakini abiria hao walipomsihi aweke gari kando kupumzika alikataa. Kamanda Twene anasema huenda hilo ndilo lililochangia kutokea kwa ajali hiyo.
Mmoja wa walionusurika na ajali hiyo Rose Anane amesema ''Nilikuwa nimelala kisha nikasikia kishindo kikubwa. Tulifanikiwa kuvunja kioo na ni baadhi yetu tu, kama watu kumi hivi ndio tuliofanikiwa kujiokoa. Ndani ya dakika kadhaa basi likashika moto watu wengine wakiwa wamenasa.''
Ajali hiyo imeibua upya wito kwa mamlaka husika nchini humo kuhakikisha kuwa watu wanatii sheria za barabarani ili kupunguza vifo na majeraha yanayotokana na barabara mbovu nchini humo. Mkazi wa eneo ilipotokea ajali hiyo Gifty Mintah amesema pamoja na kutoa malalamiko katika mikutano kuhusu kuweka matuta katika barabara hiyo. Ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara nchini Ghana,kutokana na kutofanyiwa marekebisho ipasavyo, kupuuzwa kwa sheria za barabarani pamoja na magari mabovu.
Kwa mujibu wa Idara ya Polisi ya usimamizi wa usafirishaji nchini Ghana, wastani wa watu sita hufariki dunia kila siku kutokana na ajali za barabarani. Mwezi Februari mwaka 2016, watu 70 walikufa na 13 kujeruhiwa baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika mji huo huo wa Kitampo. Mwezi Julai mwaka 2017 mmoja wa wachezaji wa klabu kubwa nchini humo ya Asante Kotoko alijeruhiwa baada ya basi lililokuwa limewabeba wachezaji wa timu hiyo kupata ajali.
Mwandishi: Angela Mdungu/ AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba