Watu 50 wafa katika ajali ya ndege Ufilipino
5 Julai 2021Idadi ya waliokufa kwenye ajali ya ndege ya kijeshi ya Ufilipino aina ya C-130 imeongezeka na kufikia 50 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na maafisa.
Uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo umeanza. Ndege ya jeshi la filipino iliyokuwa imebeba jumla ya wanajeshi 96 ilianguka jumapili katika mji wa Patikul ulioko kwenye kisiwa cha Jolo kiasi kilomita 1000 kutoka mji mkuu Manila.
Wizara ya ulinzi Jumapili ilisema wanajeshi 47 walifariki na raia wanne waliojeruhiwa wako hospitali. Msemaji wa jeshi la Ufilipino Meja Jenerali Edgard Arevalo amefahamisha kwamba tayari timu ya uchunguzi imeshafika kwenye eneo ilikotokea ajali na kwamba timu hiyo imejiandaa kubaini chanzo cha ajali hiyo mbaya.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa ndege hiyo ilizingatia utaratibu wa kuelekea kutuwa na hali ya hewa pia ilikuwa nzuri wakati wa kutuwa lakini iliacha barabara na baadae kuripuka.
Kabla ya ajali hiyo ya Jumapili rekodi zinaonesha nyingine mbaya zaidi kutokea katika ardhi ya taifa hilo ilikuwa ile ya 1971, ambayo ilitokea katika eneo la shamba la mpunga ambapo watu 40 walikufa.
Chanzo AP