Watu 5 wauawa Mogadishu kufuatia mlipuko na mashambulizi
22 Julai 2019Watu watano wanaripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mashambulizi kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Awali mashahidi walielezea kusikia mripuko mkubwa mapema asubuhi na kufuatiwa na milio mikubwa ya risasi.
Muuzaji wa duka moja mjini Mogadishu, Farah Hussein, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mripuko huo ulitokea katika eneo la kizuizi kwenye barabara ya K4 inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Mogadishu.
Hadi sasa hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda mara nyingi limekuwa likifanya mashambulizi makubwa nchini Somalia.
Nchi hiyo iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1991.