Watu 43 wauawa katika mkasa wa moto New Delhi
8 Desemba 2019Naibu mkuu wa polisi Monica Bhardwaj amesema mmiliki huyo ameshitakiwa kwa kosa la kuuwa na uzembe kuhusiana na moto huo. Mkurugenzi wa kiwanda hicho pia ametiwa mbaroni, lakini haijabainika kama ameshitakiwa au la. Moto huo ulizuka mapema leo katika jingo la ghorofa nne la eneo la Anaj Mandi, ambako zaidi ya wafanyakazi 60 walikuwa walikuwa wamelala katika vyumba hivyo, amesema msemaji wa polisi MS Randhawa.
Radhawa amasema zaidi ya watu 60 waliondolewa kwenye kiwanda hicho, 43 kati yao wakifariki dunia hasa kutokana na kuvuta moshi wenye sumu. Ameongeza kuwa karibu watu 15 hadi 20 wanatibiwa katika hospitali zilizo karibu. Randhawa amesema polisi wawili na zimamoto wawili pia wameathirika katika mkasa huo na wako hospitalini.
Waziri mkuu wa India Narendra Modi amesema kwenye ukurasa wa Twitter kuwa "Moto uliotokea katika eneo la Anaj Mandi kwenye barabara ya Rani Jhansi ni wa kutisha.”
Afisa kutoka Idara ya Zimamoto amesema kiwanda hicho – ambacho ni mrundiko wa karakana katika ghorofa kadhaa zilizotumika kutengeneza mabegi ya shule na bidhaa nyingine za plasitiki – hakikuwa na vibali vinavyohitajika vya usalama.
Chanzo haswa cha moto huo kitafahamika baada ya uchunguzi kukamilika katika siku saba, amesema Waziri Kiongozi wa Delhi Arvind Kejriwal. Aidha ametangaza fidia ya rupee milioni moja ambazo ni karibu dola 14,000 kwa jamaa za wahanga waliokufa na rupee 100,000 kwa kila mmoja aliyejeruhiwa.
Ajali na matukio ya moto hutokea mara kwa mara nchini India, ambako viwango vya usalama aghalabu hupuuzwa. Mkasa wa leo wa moto kiwandani ndio mbaya zaidi kutokea katika mji mkuu wa India tangu watu 59 walipouawa katika mkasa wa moto mwaka wa 1997 kwenye ukumbi wa sinema. Mnamo Februari mwaka huu, karibu watu 17 waliuawa katika moto uliozuka kwenye hoteli moja ya mjini Delhi.