Watu 42 wafariki Haiti kwenye maporomoko na mafuruko
6 Juni 2023Takriban watu 42 wamekufa na wengine 11 hawajulikani waliko nchini Haiti baada ya mvua kubwa kunyesha mwishoni mwa juma na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi. Hayo yameelezwa jana na maafisa wa ulinzi wa raia. Kulingana na Umoja wa Mataifa, mvua hizo zimewaathiri watu 37,000 na kupelekea wengine 13,400 kuyahama makazi yao. Mji wa Leogane, ulioko kilomita 40 kusini-magharibi mwa mji mkuu Port-au-Prince, umeathirika vibaya na uharibifu uliosababishwa na kufurika kwa mito mitatu. Waziri Mkuu Ariel Henry ameanzisha Kituo cha Kitaifa cha Operesheni ya Dharura. Hali mbaya ya hewa iliripotiwa katika Majimbo saba kati ya 10 nchini Haiti ambayo tayari yametumbukia katika mzozo wa muda mrefu wa kibinadamu unaochochewa na ghasia za magenge, kusambaratika kwa mfumo wa kisiasa na kudorora kwa uchumi.