Watu 35 wauawa katika mashambulio ya mabomu Iraq
6 Aprili 2010Watu 35 wameuwawa huku wengine 140 wakijeruhiwa kwenye mashambulio sita tofauti ya mabomu katika mji mkuu wa Baghdad katika muda wa siku tatu mtawalia yanayozusha hofu ya kurejea kwa waasi kutokana na hali ya kisiasa hivi sasa nchini humo.
Miripuko hii imetokea wakati ambapo viongozi nchini Iraq wanangang'ania mabisahano yao ya kuunda serikali, baada ya chaguzi kuu zilizomalizika mnamo Machi 7 ambazo zilishindwa kutoa mshindi mkuu.
Milipuko hio imeharibu nyumba 7 katika mitaa inayoishi watu wengi wa madhehebu ya kishia, huku, kwa mujibu wa msemaji wa idara za usalama nchini humo, Meja Jenerali Qassim Atta, nne kati ya hizo sita zimeripuka ndani ya majengo hayo.
Vingora vya magari ya kubebea wagonjwa vilisikika huku wahudumu wa afya wa dharura wakionekana kumiminika katika eneo la Allawi liliopo Baghdad ya kati , wakitoa huduma za kwanza kwa waathiriwa wa miripuko hiyo.
Wapita njia nao pia walionekana kufika sehemu hiyo kusaidia katika kuokoa watu walionusurika wa miripuko hiyo.
Afisa mmoja wa jeshi wa Allawi ameeleza kuwa siku tatu nyuma watu wawili wasiojulikana waliomba kukodisha mojawapo ya maduka yaliyomo kwenye jengo moja lililoripuliwa, na siku ya pili watu hao walionekana kuingiza mashini ambazo zinashukiwa kusababisha miripuko hiyo ambapo inasemekana ilisikika kutoka kwenye duka hilo lililokodishwa.
Miripuko miwili zaidi ilitokea katika eneo la Shurta Rabiyah liliopo Baghdad magharibi ambayo ina kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani wa kaskazini mwa mji huo mkuu.
Miripuko mingine ilishuhudiwa katika eneo la Shuala na Al Amil. Miripuko hii imetokea baada ya miripuko mingine ya kujitoa mhanga kutokea kwenye magari yaliyokuwa karibu na ubalozi za Uingereza, Iran, Misri, Ujerumani, Spain na Syria yaliyosababisha vifo vya watu 30 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 200 mnamo siku ya Jumapili.
Waziri wa mambo ya nje nchini humo, Hoshyar Zebari, aliyesema kwamba miripuko ya jumapili yalihusishwa na kundi la Al Qeada, ameeleza kuwa nia ya makundi hayo jumla yalikuwa na lengo la kupinga kuundwa serikali mpya nchini humo.
Zebari amesema kwamba hili ni shambulizi la kisiasa lililo na lengo la kutuma ujumbe, huku kukisubiriwa kuundwa serikali hiyo mpya.
Hapo awali, maafisa wa usalama walikwisha toa tahadhari ya waasi kuchukua fursa ya kuleta vurugu nchini humo kutokana na pendekezo la kuundwa serikali ya mseto.
Ijapokuwa visa vya mashambulio ya waasi vimepungua nchini humo kati ya mwaka 2006 na 2007, takwimu zilizotolewa alhamisi wiki jana zimeonyesha kwamba Wa- Iraqi 367 wameuwawa katika vita tangu mwezi jana.Hii ikiwa ndio idadi kubwa zaidi katika mwaka huu.
Mwandishi :Maryam Abdalla/AFPE
Mhariri: Othman Miraji