1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 25 wauwawa Afghanistan

6 Septemba 2016

Majeshi ya ulinzi ya Afghanistan yamefikisha mwisho mapambano ya masaa 11 katikati ya mji mkuu Kabul leo, na kumuua mtu wa mwisho aliyekuwa na silaha akipambana na majeshi hayo.

https://p.dw.com/p/1JwIA
Afghanistan Kabul nach Anschlag
Afghanistan baada ya shambulio la kujitoa muhangaPicha: picture-alliance/dpa/H. Sabawoon

Baada ya shambulio ambalo lilianza baada ya mshambuliaji aliyekuwa katika gari kujiripua katika eneo la kibishara na makaazi ya watu , watu 24 waliuwawa karibu na jengo la wizara ya ulinzi.

Polisi walilifunga eneo la kati la mji mkuu Kabul na walipambana na washambuliaji watatu ambao walijificha ndani ya ofisi ya shirika la kutoa misaada la Care International.

Afghanistan Kabul nach Anschlag
Magari ya kubebea wagonjwa yakichukua watu waliojeruhiwa mjini KabulPicha: picture-alliance/dpa/Hedayatullah Amid

Baada ya masaa kadhaa ya mapambano , yakiingiliwa mara kwa mara na milio ya risasi, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Sediq Sediqqi alisema vikosi maalum vya jeshi la Afghanistan vimewauwa wale wote waliohusika katika mashambulizi katika eneo la Share Naw katika mji wa Kabul.

Hakuna aliyedai kuhusika mara moja

Hakukuwa mara moja na madai ya kuhusika na shambulio hilo, ambalo lilifanyika masaa machache tu baada ya washambuliaji wa kujitoa muhanga wa kundi la Taliban kuwauwa kiasi watu 24 karibu na wizara ya ulinzi , ikiwa ni pamoja na idadi kadhaa ya maafisa waandamizi wa jeshi.

Ripoti za awali za watu waliofariki zinaonesha kuwa mtu mmoja aliuwawa na wengine sita walijeruhiwa wakati zaidi ya watu 31 waliondolewa kutoka mahali hapo.

Mashambulizi hayo yanaashiria hali tete ya usalama katika mji huo mkuu mwezi mmoja tu kabla ya mkutano mjini Brussels ambako wafadhili wa kimataifa wanatarajiwa kutoa ahadi zao za kuendelea kuisaidia kifedha Afghanistan.

Afghanistan Kabul nach Anschlag
Gari ya polisi iliyoharibika baada ya shambulio la kujitoa muhangaPicha: picture-alliance/dpa/Hedayatullah Amid

Baada ya masaa kadhaa ya usiku tulivu , milio ya risasi na miripuko ilisikika majira ya alfajiri.

Rafi Ullah , mlinzi wa usalama karibu na ofisi za Care International alikuwa akitembea katika eneo hilo kabla ya kusikia mripuko mkubwa. Mkaazi katika eneo hilo ambaye alijeruhiwa katika shambulio hilo Toghrul Big alisema.

"Wakati ulipotokea mripuko , madirisha yetu yote yalivunjika na kwa dakika moja nilifikiri kwamba nyumba yetu imetuangukia. Nilijeruhiwa mkononi."

Taliban

Masaa kadhaa kabla ya shambulio hilo katika ofisi za Care International usiku wa Jumatatu, kiasi ya watu 24 waliuwawa na wengine 91 walijeruhiwa wakati miripuko miwili iliyotokea kwa kufuatana ilipotokea katikati ya makundi ya watu katika eneo lenye shughuli nyingi karibu na wizara ya ulinzi.

Kundi la Taliban haraka lilidai kuhusika na shambulio hilo, ambapo mshambuliaji wa kujitoa muhanga alifanikiwa kuwauwa wafanyakazi wa wizara ya ulinzi na raia wa kawaida ambao walikimbia kuwasaidia wahanga na majeruhi wa mripuko huo.

Afghanistan Angriff auf Wohnanlage für Ausländer in Kabul
Wanajeshi wakilinda doria baada ya shambulio la kujitoa muhangaPicha: Reuters/O. Sobhani

Jenerali wa jeshi na makamanda waandimizi wawili wa polisi ni miongoni mwa waliofariki , alisema afisa wa wizara ya ulinzi. Afisa mwingine alisema naibu mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais Ashraf Ghani pia aliuwawa.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga