Kwenye majira ya saa mbili za usiku jana Jumatatu, wapiganaji wa ADF, kundi la uasi kutoka Uganda waliingia katika kijiji cha Mwenda, na kuwauwa wakaazi, wakiingia mlango kwa mlango.
Mauwaji hayo yametokea, wakati ni mchana tu, ndio miili mingine ishirini na moja ya wakaazi wa Loselose na Lohulo waliouawa na ADF ilizikwa na wanachama wa sjirika la msalaba mwekundu. Miongoni mwa miili hiyo ambayo ilikuwa imeharibika tayari, ulikuwemo wa chifu wa kijiji cha mahali.
Ripoti hiyo ilithibitishwa na mkuu wa wilaya ya Beni Donat Kibwana, anayewaomba wakaazi wa Loselose, kijiji kilichotekwa wiki iliyopitwa na ADF, waliokifanya kuwa moja wapo ya ngome zao, kabla ya kufurushwa toka kijiji hicho na majeshi ya serikali ijuma ya wiki iliyopita.
Mkuu huyo wa wilaya ya Beni Donat Kibwana amewaomba wakaazi wa Loselose kutorudi makwao, na kusubiri amri itakayotolewa na majeshi ya serikali, baada ya majeshi ambayo yanaendelea na operesheni za safishasafisha, katika viunga vya Loselose.
"Ndugu zetu waliouawa na ADF Loselose wamezikwa tayari. Nawapa pole wakazi wa Loselose na nawaomba wasirudi Loselose, na wasubiri ruhusa kutoka kwa majeshi kabla ya kurudi makwao." amesema Kibwana
Shambulizi la Mwenda, ni moja wapo ya mkururo wa mashambulizi ya ADF katika wilaya ya Beni, hasa katika Sekta ya Ruwenzori, eneo ambalo lilikuwa bado tulivu, na lililokuwa linalisha mji wa Beni.
Vyakula vinavyouzwa katika masoko ya Beni, vinatokea katika mashamba kwenye Sekta ya Ruwenzori ambayo kwa sasa inashuhudia mauwaji yanayofanywa na ADF.
Njaa kubwa huenda ikaingia Beni, ikiwa majeshi ya serikali pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa Monusco hayatowatokomeza waasi wa ADF kwani, kwa sasa wakaazi wa Mutwanga, Lume, Mwenda, Loselose na kadhalika, wameyahama makaazi yao, na kukimbilia mahala pengine.