1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 20 wauwawa katika uvamizi wa jengo la maduka Nairobi

21 Septemba 2013

Watu wenye silaha wavamia jengo la maduka mji mkuu wa Kenya Nairobi (21.09.2013) na kuuwa takriban watu 20 na kujeruhi wengine zaidi ya 50 kwa kile serikali inachosema linaweza kuwa shambulio la kigaidi.

https://p.dw.com/p/19lbu
Wafanya manunuzi walikimbia jengo la Westgate. (21.09.2013).
Wafanya manunuzi walikimbia jengo la Westgate. (21.09.2013).Picha: Reuters

Watu wengine wengi walikimbilia barabarani, madukani na sinema kusalimisha maisha yao.Kundi la wanamgambo wa Somalia la Al Shabaab lilikuwa limetishia kushambulia jengo hilo la maduka la Westgate ambalo ni mashuhuri kwa jumuiya ya wataalamu wa kigeni mjini humo.Lakini hakuna kundi lililodai mara moja kuhusika na shambulio hilo na Al Shabaab imekataa kuzungumzia shambulio hilo.

Helikopta za polisi zilikuwa zikizunguka juu ya anga ya eneo la jengo hilo wakati polisi wakisikika wakipiga makelele wakitaka watu watoke nje ya jengo hilo na huku watu wengi waliokuwa wakifanya manunuzi wakilikimbia jengo hilo.Moshi ulikuwa ukifuka kwenye mlango wa jengo hilo na watu walioshuhudia tukio hilo wamesema walisikia miripuko ya maguruneti.

Wengine wamesema wamewaona watu watano wenye silaha wakilivamia jengo hilo la maduka la Westgate na kwamba linaonekana kuwa ni shambulio na sio wizi wa kutumia silaha.

Milio ya risasi ilikuwa ikisikika kutoka hapa na pale ikiwa ni saa mbili baada ya mashambulio ya risasi kuanza wakati polisi ikilipekuwa jengo hilo wakiwasaka washambuliaji kutoka duka moja hadi jengine.

Watu wanashikiliwa mateka

Baadhi ya vituo vya televisheni nchini humo vimeripoti kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wameshikiliwa mateka lakini hakuna uthibitisho rasmi kutoka serikalini.

Wanawake wakikumbatiana nje ya jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi. (21.09.2013).
Wanawake wakikumbatiana nje ya jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi. (21.09.2013).Picha: picture-alliance/AP

Yukeh Mannaseh ambaye alikuwa ghorofa ya juu ya jengo hilo wakati mashambulizi hayo ya risasi yalipoanza amekaririwa akisema "Hawaonekani kama majambazi,hilo sio tukio la wizi". Ameendelea kusema kwamba "Inaonekana kama ni shambulio.Walinzi waliowaona wamesema walikuwa wakifyatuwa risasi ovyo."

Shahidi mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Taha amesema amesikia milio ya breki za gari iliofuatiwa muda mfupi baadae na mripuko na milio ya risasi katika ghorofa ya chini ya jengo hilo.Mtu mwengine aliyenusurika katika shambulio hilo amesema amepigwa risasi na mtu mwenye sura ya Kisomali.

Baadhi ya watu waliokuwa wakifanya manunuzi kwenye jengo hilo walikimbilia ngazini na kwenye lifti na kujicha kwenye ukumbi wa sinema wa jengo hilo wakati wengine polisi iliwagunduwa wakiwa wamejificha chooni kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.

Takriban watu 24 waliojeruhiwa walitolewa nje kwa machela na vigari vya kufanyia manunuzi.Wengi wa wahanga walikuwa na majeraha mengi madogo madogo waliyoyapata kutokana na vitu vilivyorushwa kutokana na mripuko.Wengine walitoka nje wakitembea wenyewe kwa miguu huko nguo zao zilizorowa damu zikifunika majeraha yao.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limeliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba takriban watu 15 wameuwawa na kuna uwezekano wengine waliouwawa bado wangaliko ndani ya jengo hilo.Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Kenya Abbas Gullet amesema idadi ya maafa na majeruhi ni kubwa na ile waliyokuwa nayo ni ya wale walioko nje. Gullet alitowa kauli wakati milio ya risasi ilipokuwa ikiendelea kurindima ndani ya jengo hilo.

Kuna maafa ndani ya jengo

Kenya imekuwa ikilaumu kundi la al Shabaab na wafuasi wao kwa mashambulio kadhaa ya risasi, mabomu na maguruneti dhidi ya makanisa na vikosi vya usalama tokea jeshi la Kenya lilipoingia Somalia kusaidia kupambana na wanamgambo wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda miaka miwili iliopita.

Polisi akiwa ndani ya jengo la madula la Westgate mjini Nairobi.(21.09.2013).
Polisi akiwa ndani ya jengo la madula la Westgate mjini Nairobi.(21.09.2013).Picha: Reuters

Al Shabaab huko nyuma ilitishia kushambulia majengo ya ghorofa refu mjini Nairobi na maeneo ya starehe na burudani vikiwemo vilabu vya usiku kucha na mahoteli ambayo hupendelewa na watu wa mataifa ya magharibi walioko katika mji mkuu huo. Lakini hadi sasa wameshindwa kufanya mashambulizi ya aina hiyo.

Mwanajeshi mmoja wa zamani wa Uingereza aliyekuweko katika eneo hilo amesema yeye mwenyewe binafsi aliyapapasa macho ya watu wanne na walikuwa tayari wamekufa akiwemo mtoto mmoja.

Amesema kuna mauaji makubwa kwenye jengo hilo.

Mwanamgambo mmoja wa jeshi la serikali alipoulizwa iwapo hilo lilikuwa ni tukio la wizi amejibu "Hapana huo ni ugaidi".Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kutoka kwa polisi kuhusiana na dhamira ya washambuliaji hao.

Polisi akiwa ndani ya jengo la madula la Westgate mjini Nairobi.(21.09.2013).
Polisi akiwa ndani ya jengo la madula la Westgate mjini Nairobi.(21.09.2013).Picha: picture-alliance/AP

Polisi imelizingira jengo na barabara zilioko karibu na jengo hilo lilioko kwenye kitongoji cha Westlands katikati ya mji wa Nairobi.Wizara ya mambo ya ndani imesema huenda hilo ni tukio la kigaidi na tayari jeshi la Kenya limefika katika eneo la mkasa kushirikiana na polisi kudhibiti hali hiyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri:Caro Robi