1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 19 wauwawa katika shambulizi Kabul

2 Novemba 2021

Watu wapao 19 wameuawa na wengine 50 wamejeruhiwa katika shambulizi lililolenga hospitali ya kijeshi mjini Kabul, tukio hilo likiwa la hivi karibuni kabisa kuitikisa Afghanistan tangu Taliban ipochukua madaraka

https://p.dw.com/p/42U2j
Kabul, Afghanistan | Explosionen in der Nähe von Militärkrankenhaus
Picha: Sayed Khodaiberdi Sadat/AA/picture alliance

Kulingana na Taliban shambulizi hilo limetokea baada ya mshambuliaji wa kujitoa muhanga kujiripua karibu na mlango na kufuatiwa na watu wengine waliojihami kwa silaha kuingia ndani ya hospitali hiyo na kufyatua risasi.

Afisa katika wizara ya afya ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa miili 19 na majeruhi 50 wamepelekwa katika hospitali za mjini Kabul. soma Zaidi ya watu 30 wauawa Afghanistan

Kwa takriban miaka 20 Taliban ilikuwa ikiendesha uasi dhidi ya serikali iliyoondolewa madarakani na ambayo ilikuwa inaungwa mkono na Marekani lakini sasa ni wao wanaokabiliwa na shinikizo la kuleta utulivu nchini humo kufuatia msururu wa mashambulizi yanayofanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS).

Hospitali hiyo ambayo huwahudumia wapiganaji wa Taliban pamoja na vikosi vya zamani vya usalama vya serikali, iliwahi kushambuliwa mnamo mwaka 2017 wakati watu waliojifanya kuwa madaktari walipoishambulia na kuwauwa watu 30.

Hakuna aliyedai kuhusika

Afghanistan Kandahar Selbstmordattentat des IS auf Schiiten-Moschee
Picha: Shiite Coordination Council of Afghanistan

Hakuna kundi lolote lililojitokeza kudai kuhusika na shambulizi la leo, lakini IS ilidai kuhusika na mashambulizi mengine manne tangu Taliban ilipoingia madarakani mnamo Agosti 15, ikiwa ni pamoja na shambulizi la kujitoa muhanga lililolenga msikiti wa waislamu wa dhehebu la Shia. Kundi hilo linawachukulia Washia kama wazushi.

Hata hivyo manusura wa shambulizi hilo wameliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji walikuwa wakiimba "Taliban iishi kwa muda mrefu" kwa lugha ya Pashtun na kushambulia hospitali yote isipokuwa wadi mbili zilizopo mwanzo wa jengo hilo ambazo zinawahudumia wagonjwa wa Taliban.

Msaada kwa Waafghani

Afghanistan Kabul Angelina Jolie
Picha: UNHCR/Jason Tanner

Huku haya yakijiri Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi, UNHCR, limeanza kusafirisha misaada kuelekea mjini Kabul ili kusaidia maelfu ya Waafghani waliopoteza makaazi yao kujenga makao mapya kabla ya kuanza kwa msimu wa baridi kali.

UNHCR imesema ndege ya kwanza inatarajiwa kuwasili Kabul baadaye leo Jumanne, iliyobeba tani 33 za vifaa vya ujenzi wa muda. Ndege zingine mbili zinatarajiwa kuwasili Novemba 4 na 7.

Takriban watu milioni 3.5 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na ghasia na migogoro nchini

Afghanistan, ikiwa ni pamoja na watu laki 7 waliokimbia mwaka huu. UNHCR inanuia kuwapa msaada watu laki 5.

 

AFP/dpa